Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wazee Mto wa Mbu wapata mkombozi

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Shirika la Uzee na Furaha limeanzishwa katika mji wa Mto wa Mbu jijini Arusha ili kuwasaidia wanawake wazee katika mji huo ambao wamekuwa katika tishio la kufanyiwa ukatili na kuuawa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Februari 25, 2019 mkurugenzi wa shirika hilo, Jackline Samson amesema kwa kushirikiana na marafiki zake wa nchini Ireland  wameamua kuwasaidia wazee, wanawake na wanaume ambao wanataabika katika mji huo.

Amesema kwa sasa zaidi ya wazee 20 wameanza kupewa huduma mbalimbali majumbani baada ya kutambuliwa na baadaye ambao hawana ndugu watapata hifadhi.

"Tayari tumejenga jengo maalum la kuwasaidia wazee, kwa sasa tunawapa huduma mza afya na chakula nyumbani na taratibu zikikamilika ikiwepo upatikanaji wa fedha baadhi tutawahamishia kituoni," amesema

Fatuma Adam (86) mkazi wa Mto wa Mbu Mnadani ambaye hivi karibuni, alinusurika kuuawa na vijana wanaofanya matukio ya ukatili, amesema wanashukuru kwa misaada ya kituo hicho cha kulea wazee.

"Mimi nilifanyiwa ukatili na hadi sasa nimekuwa napatiwa matibabu tunashukuru Mungu kupatiwa msaada wa huduma za afya na chakula na tunaomba usaidizi zaidi, lakini pia polisi wakamate wahusika wanaotuwinda," alisema.

Ofisa Ustawi wa jamii, tarafa ya Manyara, Swedi Kiluvia amesema kuanzishwa kwa kituo cha kulea wazee katika mji huo ni faraja kwa wazee kwani sasa watakuwa na uhakika wa maisha yao.

"Tatizo lilipo tuna idadi kubwa ya wazee ambao walikuja miaka mingi iliyopita katika mji huu kufanya kazi na baadhi hawana ndugu sasa wamekuwa wakihangaika kujimudu kimaisha," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz