Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake watakiwa kupambana kusaka mafanikio

Wanawake watakiwa kupambana kusaka mafanikio

Wed, 30 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya kuwepo kwa kampeni nyingi za usawa na kijinsia, imeelezwa kuwa hakuna njia ya mkato kuelekea katika mafanikio zaidi ya kujiendeleza kielimu na kujituma katikia shughuli mbalimbali.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba30, 2019  jijini Dar es Salaam na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Lindam Group, Zuhura Muro na kubainisha kuwa kinachowakwamisha wanawake ni mfumo dume, ikiaminika kuwa hawawezi kuwa viongozi.

 “Nyingine ni kujihukumu wenyewe kwamba mwanamke akipewa nafasi anabaki kujiuliza kweli nitaweza? Anaanza kujipa wasiwasi yeye mwenyewe na akipata sauti inayompa wasiwasi ndiyo anashindwa kabisa,” amesema Muro.

Zuhura aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya Mwananchi Communication’s Ltd (MCL) amewataka wanawake wajiandae kuwa viongozi kielimu na kuwa na bidii ya kazi.

“Wanawake wajue hawatapewa nafasi kwa sababu wao ni wanawake lazima wajiandae. Mwanamke aangalie elimu yake na vigezo vya kitaaluma, kujituma na kujiendeleza lazima uwe na upekuzi uangalie dunia inakwenda wapi,” amesema.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akitaka wanawake wajitume zaidi kazini.  

 “Niwe mkweli naamini hakuna mwajiri au kampuni yoyote inayoweza kukupa kazi au cheo kwa sababu wewe ni mwanamke ni mpaka ulete matokeo mazuri, ni mpaka uonyeshe uwezo wako,” amesema Zaipuna.

Chanzo: mwananchi.co.tz