Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake watakiwa kuinuana ili kufikia usawa wa Kijinsia

47238 SERENGETI+PIC

Tue, 19 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanawake nchini wametakiwa kutumia vizuri nafasi walizonazo kwa kuwainua wenzao ambao wana ujuzi wa kiutendaji ili kupanua wigo katika kufikia usawa wa kijinsia katika nyanja za kimaamuzi katika taasisi mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL), Helene Weesie wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika Ijumaa Machi 15, 2019 jijini hapa.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikiweka mkazo katika kuwainua wanawake katika nafasi mbalimbali ili kufikia usawa wa kijinsia kwakuwa mwanamke ana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika jamiii na taasisi.

Mbali na Dar es Salaam maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanda vilivyopo Mwanza na Moshi kupitia jukwaa maalumu la wanawake kwa lengo la kujadili mchango wao katika kuendeleza taasisi na jamii.

 “Wanawake wamekuwa msingi mkubwa katika nyanja za ufanyaji maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi maeneo ya kazi hivyo kuna haja ya kutoa nafasi kwa wanawake wengi zaidi kwenye taasisi zetu ili kufikia usawa wa kijinsia na zaidi kufikia maendeeleo endelevu,” alisema Weesie.

Usawa wa kijinsia umehimizwa katika maadhimisho ya mwaka huu kupitia kauli mbiu isemayo “Badili Fikra kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu”.

Hatahivyo, Mkurugenzi huyo aliwataka wanawake kujiamini zaidi ili waweze kupata nafasi za juu huku akihimiza kutosita kuonyesha ujuzi walionao kwani ndiyo msingi wa mafanikio.

Naye, Mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) Mary Rusimbi alisema wanawake wameendelea kushiriki kwa kasi katika ngazi za uongozi katika jamii na taasisi na kwamba hiyo ni ishara nzuri katika kuufikia usawa wa kijinsia hapa nchini.

Aliipongeza Kampuni ya bia ya Serengeti kwa kutoa kipaumbele kwa wanawake na kuwapa jukwaa maalumu la wanawake liitwalo ‘SBL Spirited women’ ili kutoa nafasi ya kuboresha utendaji wao.

“Wanawake ni viongozi sio tu katika kuongeza tija lakini ni viongozi katika kushika shirika likae pamoja na kuongeza ufanisi wa kazi wanazozifanya endapo ujuzi wao utatumika vizuri,” alisema Rusimbi.



Chanzo: mwananchi.co.tz