Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wanaoficha madini sehemu za siri waonywa

45645 Pic+siri Wanawake wanaoficha madini sehemu za siri waonywa

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Umoja wa Wanawake Wachimbaji Madini ya vito nchini (Tawoma) Tawi la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamewataka wanawake wanaoficha madini kwenye sehemu zao za siri kuachana na mtindo huo kwani ni ukwepaji kodi na una athari kiafya.

Mwenyekiti wa Tawoma tawi la Mirerani, Rachel Njau ameyasema hayo leo Machi 8 kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite.

Njau amesema kumekuwepo na udanganyifu miongoni mwa wanawake ambao huficha madini kwenye miili yao bila kujua athari zake kwa baadaye na kusababisha Taifa kukosa mapato.

Amesema wanalikemea jambo hilo kwa kila mwanamke na kulipinga kwa nguvu zote kama viongozi wa wanawake wachimbaji madini wa mkoa wa Manyara.

"Tunaiomba Serikali kuwachukulia hatua wote watakaokutwa na uhalifu huo, tunapendekeza wakipatikana washtakiwe mahakamani na kisha wapigwe picha na majina yao yaandikwe ili wasiruhusiwe kuingia tena ndani ya ukuta," amesema Njau.

Kwa upande wake, ofisa madini mkazi wa mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima amesema baadhi ya wanawake wanaofanya vitendo hivyo hawajapatiwa elimu ya madhara ya wanachokifanya.

Ntalima amesema hivi sasa Rais John Magufuli amefuta kodi nyingi za madini hivyo kinacholipwa ni kidogo na kwa mantiki hiyo hakuna sababu ya kutorosha madini.

Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara, (Marema) Tawi la Mirerani, Dk Curtius Msosa amesema kitendo cha kutorosha madini kwa kuingiza sehemu za siri kinasababisha madhara ya kiafya.

Dk Msosa amesema kuingiza madini sehemu za siri kunasababisha bakteria waingie mwilini hivyo kupata magonjwa ikiwemo kansa ya kizazi.

Mmoja kati ya wauza matunda na mama lishe, Deshfose Solomon amesema baadhi ya wanawake wamesababisha wao kuangaliwa kwa umakini kutokana na kutumika kuficha madini.

Mwanamke mchekechaji wa eneo hilo, Naa Mamasita amesema wanawake wanaofanya vitendo hivyo waachane navyo kwani wanawadhalilisha wanawake wenzao.

 

 

MWISHO



Chanzo: mwananchi.co.tz