Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake walia rushwa ya ngono kupata uongozi

SEXUAL.png Wanawake walia rushwa ya ngono kupata uongozi

Mon, 29 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WANAWAKE wa kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Ukonga jijini Dar es Salaam, wamesema kuwa tatizo la rushwa ya ngono limeendelea kuwa kikwazo kwa wanawake wengi kushindwa kupata nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali.

Walitoa kauli hiyo katika semina maalum jijini Dar es Salaam, iliyolenga kuwapatia elimu wanawake hao namna ya kupambama na vitendo hivyo vya ukatili iliyodhaminiwa na Taasisi ya Women Fund.

Lucy Makula, Msaidizi wa kisheria Kipunguni na Mjumbe wa Sauti ya Jamii, alisema tatizo hilo la rushwa limekuwa likiwakatisha tamaa wanawake wengi wanapoomba ajira katika taasisi mbalimbali na pia katika nafasi ya uongozi kwenye siasa.

“Sijui kama jambo hili litaisha, wanawake tumekuwa tukipambana sana lakini tunarudishwa nyuma na watu wasiotutakia mema, kuna shuhuda nyingi sana za wanawake au wasichana kuomba rushwa ya ngono wanapokwenda kuomba nafasi za ajira na wengi wanakosa kwa sababu ya kukataa kutoa rushwa hiyo,” alisema Makula.

“Kwenye siasa ndiyo usiseme, huko tena ndiyo hatari. Angalau msichana mwenye umri mdogo anaweza kufikiriwa kupewa nafasi kwa lengo la kwamba aingie ili wamuombe rushwa ya ngono au wanapendekeza jina lake halafu wanajitokeza watu kila mmoja kwa wakati wake wanakuwa wanamshawishi atoe rushwa ili wampitishe.”

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Kata za Msongola na Kivule, Msekwa Joliga, alisema wamekuwa wakipokea kesi nyingi zinazohusiana na rushwa ya ngono.

“Ni kweli tunapata kesi nyingi za ambazo wanawake na wasichana wamekuwa wakija kulalamika kwamba wanaombwa rushwa ya ngono aidha na viongozi katika nyanja mbalimbali wanapokwenda kutafuta huduma au nafasi za uongozi na tumekuwa tukipambana kuyashughulikia na kuwashauri pia,” alisema Joliga.

Sheikh Abdi Mahanyu kutoka eneo hilo, alisema imefika wakati ambao wanawake nao wanahitaji kubadilika kwa kuacha kufumbia macho au kuwaficha watu wanaofanya vitendo hivyo vya unyanyasaji badala yake wahakikishe wanatoa taarifa katika vyombo vya dola ili wahusika wachukuliwe hatua.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live