Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wachimbaji watafuta mbadala kujiongezea kipato

Wanawake Geita .jpeg Wanawake wachimbaji watafuta mbadala kujiongezea kipato

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wanawake wachimbaji katika kata ya Mgusu wilaya ya Geita wamelazimika kutafuta njia mbadala ya kujiongezea kipato kutokana na kazi ya uchimbaji wanayoitegemea kuwa na ujira mdogo na kuhatarisha usalama wa afya zao.

Wanawake hao hulipwa kati ya Sh2000-5000 kwa siku kwa kazi ya kuponda mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu pamoja na kuchenjua udongo wenye mchanganyiko wa kemikali ya zebaki kazi ambazo ni hatari kwa afya zao.

Katika kuhakikisha wanapata kazi mbadala ya kuwapatia kipato shirika lisilo la kiserikali la Africa Transcribe Enterprises likishirikiana na shirika la Women African Alliance la Afrika Kusini wametoa mafunzo ya kutengeneza sabuni kwa wanawake hao ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Msimamizi wa miradi na utawala kutoka shirika la Africa Tanscribe Ninaeli Urassa, akizungumza jana Jumamosi Desemba 10, 2022 wakati wa mafunzo hayo, alisema shirika hilo lilikutana na kina mama wanaofanya kazi za kuchakata dhahabu na kuomba kujengewa uwezo wa kazi za mikono zitakazo waongezea kipato.

“Licha ya kazi ngumu wanayofanya ujira wanaopata ni kidogo lakini wanamajukumu ya malezi na muda mwingi wanautumia wakiwa machimboni kwa elimu hii wataweza kutengeneza sabubi na kuuza na kupata muda wa kukaa na watoto nyumbani na kuwapa malezi bora huku uchumi ukiimarika,” alisema Urassa

Amesema wameanza na wanawake 30 na mafunzo hayo yatatolewa kwa wakina mama zaidi ya 100 na watapatiwa elimu ya ujasiriamali na namna ya kutunza fedha ili waweze kusimamia biashara iwe endelevu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kina mama hao wa Mgusu wamesema mafunzo ya utengenezaji sabuni ni fursa ya kiuchumi kwao kutokana na wao kulazimika kufanya kazi na watoto mgongoni huku wanaobaki nyumbani wakilazimika kushinda njaa.

“Wanawake tunateseka sana tunafanya kazi na watoto mgongoni bado vumbi na hawapati chakula kwa wakati ndio maana mgusu inaongoza kwa utapiamlo kwa mafunzo haya sasa mama atakaa nyumbani na kutengeneza sababuni huku akihudumia familia,” amesema Patricia Joseph

Pendo Samson amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza kipato na kuwasaidia wanawake ambao ni walezi wa familia kumudu maisha na kusimamia malezi ya watoto.

Chanzo: Mwananchi