Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake Arusha vinara kuwapeleka watoto shule, wanaume

90910 Pic+wanawake Wanawake Arusha vinara kuwapeleka watoto shule, wanaume

Mon, 6 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Wanawake wengi katika Jiji la Arusha nchini Tanzania ndiyo wamejitokeza kupeleka watoto shule kuanza darasa la kwanza tofauti na wanaume.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi leo Jumatatu Januari 6, 2020 katika shule za msingi Uhuru, Kaloleni, Meru na Ngarenaro jijini Arusha umebaini idadi kubwa ya wanawake wakiwapo wenye watoto wachanga wamejitokeza kupeleka watoto shule tofauti na wanaume.

Janet Lyimo akizungumza na Mwananchi shule ya msingi Uhuru amesema amempeleka kumuandikisha shule mtoto wake kutokana na mume wake kuwa na majukumu mengine.

Lyimo amesema mume wake, Joseph walipanga kuongozana lakini amechelewa kuamka na ulipofika muda wa kumpeleka Mtoto akawa na ratiba nyingine.

"Mtoto angependa tuje wote ila baba yake ana kazi nyingine na hivyo alibaki nyumbani," amesema.

Amina Salehe mkazi wa Bondeni akiwa na mtoto mdogo amesema amelazika kumpeleka mwanae Amina Salim shule kwa kuwa baba yake aliondoka asubuhi kwenda kazini.

"Baba yake ameondoka mapema kwenda kazini kwa kuwa tayari amenunua daftari na sare za shule mimi nimeamua kumleta," amesema

Abubakar Mwanga anasema wanaume wengi hawajajitokeza kupeleka watoto kwani wana kazi nyingi tofauti na wanaume .

"Mimi leo siendi kazini ndio sababu nimemleta Mtoto ila naona wenzangu wanaume wana majukumu mengine," anasema

Hata hivyo, wakati wanaume wengi wakikwepa kupeleka watoto shule baadhi ya watoto wameeleza walipenda siku ya kufungua shule waambatane na wazazi wote

Ismail Juma anasema amepelekwa shule ya Meru na mama yake kuanza darasa la kwanza lakini angefurahi na baba yake angekuwapo.

"Ningependa Baba aje ila nimemuacha nyumbani nimekuja na mama "amesema

Shadiya Rajabu anasema anapenda shule na amepelekwa shule na mama yake na Baba amekwenda kazini.

Katika jiji hilo, watoto wengi zaidi ya uwezo wa shule wamepelekwa kujiandikisha darasa la kwanza.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya walimu wa shule wamesema tofauti na matarajio watoto wengi wamefikishwa na wazazi leo Jumatatu kutaka kuandikishwa darasa la kwanza na chekechea.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Meru, Jiji la Arusha, Mussa Rwambano amesema shule hiyo ilitarajia kuandikisha watoto 160 wa darasa na kwanza na 100 wa chekechea lakini idadi imekuwa kubwa.

"Tunaendelea kuwapokea hadi muda huu tayari tumeandika watoto 148 wa darasa la kwanza naona bado wapo wengi hapa na wazazi wao," amesema

Amesema shule hiyo ambayo ipo mjini tatizo kubwa na uhaba wa madarasa lakini watajitahidi kuwapokea watoto n kutoa elimu Kwa wazazi.

"Kuhusu madawati hatuna shida watoto wote 160 ambao tulipanga kuwapokea watakaa kwenye madawati," amesema

Katika shule ya Uhuru, Kaloleni na Ngarenaro shughuli za kupokea watoto kulikuwa linaendelea hata hivyo walimu walieleza wote watapokelewa.

"Hakuna mtoto ambaye atarudishwa nyumbani tutawapokea wote na baadaye tutaona utaratibu wao wa kusoma," amesema mwalimu wa shule ya Uhuru.

Hata hivyo, tayari Katibu Tawala mkoa wa Arusha, Richard Kwitega ameagiza watoto wote kupokelewa wakati jitihada za kukamilisha madarasa na madawati zikiendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz