Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaushirika Mruwia Moshi Vijijini wavurugana

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wanachama wa chama cha Ushirika wa Mazao (Amcos) cha Mruwia wilaya ya Moshi wanamuomba, Mrajisi wa Ushirika mkoa Kilimanjaro, kuingilia kati mgogoro wa uongozi katika chama hicho.

Wakizungumza na Mwananchi jana Septemba 25, 2018, baadhi ya wanachama wamedai walimchagua mwenyekiti wao, Philip Materu katika mkutano halali wa Oktoba 10, 2017, lakini hadi leo hajakabidhiwa ofisi za chama chao.

Wanachama hao wanadai aliyekuwa mwenyekiti wa Amcos hiyo kwa miaka 20, Mathias Akaro, hataki kukabidhi ofisi hiyo baada ya wanachama kuhoji mapato ya biashara ya kahawa iliyouzwa nje ya nchi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mruwia, Zakaria Njau alidai katika uchaguzi huo, wanachama walimchagua Philip Materu kuwa mwenyekiti wao lakini Kiara ameendelea kung’ang’ania madaraka.

“Tulipomchagua (Philip) kwa kura nyingi huyo Akaro hakuchaguliwa hata kwenye nafasi ya ujumbe wa bodi. Kukaletwa mizengwe tukarudia uchaguzi ndio akapata nafasi ya ujumbe” alidai Njau.

Njau alidai, pamoja na wanachama kumchagua Materu kuwa mwenyekiti wao, hadi leo inakaribia mwaka mmoja hajakabidhiwa ofisi ili atekeleze yale aliyokuwa amewaahidi wanachama.

Kwa upande wake, mwanachama wa Amcos hiyo, Emilian Maliwa, alidai msimu wa 2017/2018 hawajawahi kuelezwa chama hicho kimepata mapato kiasi gani katika biashara ya kahawa.

“Lakini keshokutwa (Ijumaa) huyu mwenyekiti ameitisha mkutano kwenye ukumbi na ametangaza watakaoingia ni wale tu wenye kadi za uanachama lakini si wanachama wote wana kadi,” alidai.

Maliwa alidai utaratibu huo wa kutumia kadi za wanachama badala ya rejista ya wanachama una lengo la kutumia nafasi hiyo kuwazuia wanachama ambao hawajapewa kadi jambo ambalo si sahihi.

Akaro alipotafutwa jana, alikanusha tuhuma za kung’ang’ania madaraka na kudai mwenyekiti aliyechaguliwa, alikumbwa na tuhuma za wizi wa kilo 24 za kahawa mali ya chama hicho.

“Huyo mwenyekiti alikumbwa na tuhuma za wizi wa kilo 24 za kahawa akasimamishwa kazi na hajarudishwa kazini ili mimi sasa niweze kumkabidhi ofisi,” alidai Akaro na kuongeza,

“Ni kweli nimeitisha huo mkutano wanaousema lakini ni kwa maelekezo ya Mrajisi wa Ushirika wa mkoa. Wanachama wasio na kadi hawataruhusiwa kufanya maamuzi watakuwa watazamaji.”

Kuhusu madai ya ubadhirifu uuzaji wa kahawa ya ubia, Akaro alikanusha tuhuma hizo na kudai kuwa kilo moja iliyouzwa mnadani kwa Sh12,000 na wanachama kulipwa Sh4,000 si ya kweli.

Materu ambaye ni mwenyekiti mpya alipoulizwa kuhusu tuhuma za wizi wa kilo 24 za kahawa, alizikanusha na kumtaka Akaro azithibitishe badala ya kueneza tuhuma za kupika.

“Hiki chama kina mhasibu, kina mlinzi na kina mtunza stoo, angewaleta waeleze kama niliwahi kuiba kahawa. Na kwa nini analeta tuhuma hizi baada ya mimi kushinda uenyekiti?”, Alihoji Materu.

Mrajisi wa Ushirika mkoa Kilimanjaro, John Henjewele hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kutokuwa hewani na mmoja wa wasaidizi wake alidai yuko kwenye ziara ya mwenge wa Uhuru.

Chanzo: mwananchi.co.tz