Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume watuhumiwa kudai mahari wakitoa talaka

Mahari Pic Wanaume watuhumiwa kudai mahari wakitoa talaka

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Aina mpya ya kichocheo cha ukatili wa kijinsia kwa wanawake imeibuka wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma, baada ya baadhi ya wanaume kutuhumiwa kudai kurejeshewa mahari waliyoilipa ndoa zinapovunjika.

Tuhuma hizo zilitolewa wilayani Bahi juzi na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Bahi, Songoro Mjongo katika tamasha la kupinga ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na Shirika la Msichana Initiatives.

“Sasa umekaa na mwanamke miaka 10 na umemzalisha, leo utamrudishia usichana wake? Acheni tabia mbaya umekaa na mwanamke umezaa naye kw anini unataka urudishiwe mahari? Mila hazipo, pindi ulichoishi anakupikia, amekuzalia watoto, kwa nini mashtaka hayo. Yakija kwetu sisi…. hatutakuacha salama,” alisema Mjongo.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mkunda aliitaka jamii, viongozi wa dini na wazee maarufu kwa pamoja kukaa chini na kuliangalia suala la mahari kwa jicho la ukatili wa kijinsia.

“Kwa sababu mahari imetumika kama kichocheo, tuone mahari kama ni sehemu ya asante kwa wazazi kwa kumlea binti lakini isiwe majadiliano kama unanunua shamba, ng’ombe mnadani,” alisema Mkunda.

Mbali na hilo, Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiatives limevunja ndoa ya utotoni iliyokuwa ifungwe Novemba 30, 2022 katika kijiji cha Babayu wilayani huo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na polisi hivi karibuni, zinaonyesha kuwa watu 15,131 walifanyiwa ukatili wa kijinsia kati ya Januari hadi Juni 2021, idadi ambayo ni wastani wa matukio 2,522 kwa mwezi na wastani wa matukio 14 kwa siku.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Bahi, Iddi Ibrahim alisema: “Si ndio nimesema (matukio) mengine yanaishia kwenye madawati ya watendaji hayafiki polisi. Nataka nilifuatilie, mimi nilikuwa silijui. Lakini kama alivyosema matukio haya huishia kwa watendaji hayafiki polisi. Hili nimekuja kulisikia hapa (kwenye mkutano)”.

Akieleza mafanikio ya hatua zilizochukuliwa wilayani humo katika kupambana na ukatili wa kijinsia, Mkurugenzi wa Msichana Initiatives, Rebeca Gyumi alisema majukwaa ya Cafe yaliyoanzishwa mwaka 2017, yamewezesha kuibuliwa kwa matukio ya ukatili wa kijinsia 404, huku kesi hizo zikipungua kwa asilimia 64.

Mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Bahi, Peasi Manzeni alisema kuwa hali hiyo inajitokeza ikiwa mwanamke amemkataa mwanamume waliyeoana na kwenda kuolewa na mwanamume mwingine.

“Kama umeoa mwanamke amekukimbia ukamtafuta ukampata, ukimhoji anakwambia mimi sikutaki. Utafanya nini badala ya kumwambia akurejeshee mahari yake,” alisema Manzeni.

Chanzo: Mwananchi