Wanaume wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwamo kupigwa na kunyimwa unyumba na wake zao majumbani, wametakiwa kwenda Polisi kutoa taarifa juu ya unyanyasaji huo wa kibinadamu katika Dawati la Jinsia, ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Kata ya Malambo Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Leyla Mhando, akiwa kwenye Kikao na Viongozi wa Serikali za Mitaa, amewataka wanaume wanaokung'utwa na kunyimwa tendo la ndoa na wake zao kutokuogopa kwenda kuripoti Polisi, ili wahusika washughulikiwe kulingana na sheria za nchi.
Amesema ukatili wa kingono, vipigo, saikolojia na ule wa kiuchumi unapaswa kudhibitiwa kuanzia ngazi ya familia, vinginevyo vinaweza kusababisha vifo na ulemavu dhidi ya binadamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanawake wametoa kilio chao pia cha kushushiwa vipigo na waume zao, wanapokuwa wamebugia chang'aa.