Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume walalamikiwa kuwatelekeza watoto walemavu

Thu, 13 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilolo.  Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah amewaasa wanaume kutowatelekeza watoto wenye ulemavu baada ya kuzaliwa, badala yake wasaidiane na wake zao katika malezi na kuhakikisha wanapewa haki ya msingi ya kupata elimu.

Pia ameitaka jamii kuacha dhana potofu kwamba kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni laana.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 13, Abdalah amesema wapo baadhi ya wanaume ambao wakipata watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiwatelekeza huku mzigo wa malezi ukiwaangukia wanawake peke yao.

Amesema kutokana na hali hiyo wameanzisha mkakati wa kuwatambua watoto wenye ulemavu wakiwa na umri wa kuanza shule ili mwakani waingie darasani.

“Hakuna mtoto mlemavu ambaye ana uwezo wa kukaa darasani atakayebaki nyumbani, wito wangu kwa wanaume, wasaidie malezi kwa kuwa watoto wengi wapo na mama zao, baba zao mpo wapi?” amesisitiza.

Ameongeza kuwa watoto wenye ulemavu ni sawa na watoto wengine na kwamba, mzigo wa malezi unaoonekana wakati wakiwa wadogo hauwezi kuisha kama watoto hao hawataandaliwa njia ya msingi ya maisha.

Awali, diwani wa Nyalubu, David Mfugwa amesema bado baadhi ya jamii inakabiliwa na dhana finyu kuhusu watoto wenye ulemavu, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita.

“Hakuna mtoto aliyependa kuzaliwa mlemavu hivyo ni jukumu letu kuwatunza, elimu finyu ndiyo inayowafanya baadhi ya wanaume kuona mzigo kuwalea watoto wao na hata kuwasomesha,” amesema.

Mama wa mtoto mwenye ulemavu, Faraja Enock amesema baba wa mtoto wake alimkataa mwanae mara baada ya kubaini kuwa amezaliwa na ulemavu wa viungo.

“Kwa hiyo mpaka leo namlea mwanangu peke yangu ila naamini mtoto huyu akisoma na kuja kuwa na maisha mazuri baba yake atarejea, saa hizi anahisi kama huu ni mzigo kumbe huyu ni mtoto kama walivyo wengine tu,” amesema Faraja.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz