Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume ‘teleza’ waanza kudakwa

60069 TELEZA+PIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga ametangaza operesheni ya kuwasaka wanaume wanaojipaka oil chafu ‘wanaume teleza’ kisha kuwabaka wanawake mkoani humo.

Katika kutekeleza operesheni hiyo, mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma, Raphael Mayunga alisema jana kuwa jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa kwa tuhuma hizo na kuwaomba wananchi kufika ili wawatambue, “hata hapa kwenye kikao ninazo picha za hao vijana, njooni muwatambue, kama kuna mtu anaogopa anaweza kunifuata kwa siri aje awatambue,” alisema.

Oparesheni hiyo inaendeshwa na askari polisi ambao wanafanya msako katika mitaa mbalimbali ya Kigoma Ujiji huku Anga akiliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha vilabu vya pombe za kienyeji vinafunguliwa saa 11 jioni na kufungwa saa nne usiku.

Wanaume teleza ni jina linalotumika kuwatambulisha vijana wanaofanya vitendo vya uhalifu nyakati za usiku ambao huvunja milango, kuiba na kubaka wanawake.

Jana, Anga alifanya ziara katika Kata ya Mwanga Kusini ambako vitendo vya ubakaji vimetamalaki na kusema, “hili suala la teleza nimelisikiasikia muda mrefu tangu nimekuja (Kigoma mwaka 2016) lakini sikujua kama ni kubwa kwa kiwango mnachoeleza, watu wanazungumza kuhusu teleza kana kwamba sio jambo kubwa. Kina mama mnaniomba niwasaidie hawa teleza wakamatwe, nawahakikishia huyu teleza atakoma. Kabla sijaondoka Kigoma nitahakikisha teleza wamekwisha na msingi nitakaouweka hata akija mkuu wa wilaya mwingine hatopata shida,” alisema Anga.

“Nataka hawa teleza wanapokamatwa wakifikishwa Polisi wapigwe fimbo nyingi sana na wanapokwenda mahakamani wafungwe, nawaambia wataozea jela.”

Pia Soma

Wakati Anga akieleza hayo, juzi kanisa halisi la Mungu baba lilifanya maombi maalumu kwa ajili ya kuomba wanaume teleza wateketezwe.

Mkazi wa Mwanga Kusini, Nunu Mzila ambaye aliwahi kuingiliwa na teleza mara sita na mara nne kati ya hizo kushambuliwa kwa kukatwa mapanga kichwani, mikononi na mgongoni, alisema, “wameshanigeuza nunu mzila (mboga yao), wakati mwingine wanapitia hadi pesa zangu wakati mimi ndio baba na ndio mama, nikizidi kuongea najisikia hadi kulia kwa uchingu,” alisema na kuangua kilio wakati wa mkutano huo.

Juzi, akiongoza maombi hayo katika ibada ya hija iliyofanyika katika Uwanja wa Mwanga Center, Baba Mtakatifu wa Kanisa halisi la Mungu baba, Elisha Elia alisema tatizo la wanaume teleza sasa limekwisha.

Alisema vijana wanaovunja milango na kutesa watu hasa kina mama haliwezi kuachwa liendelee na kila mmoja anapaswa kuomba Mungu ili roho ya dhambi ishindwe. “Hawa teleza wanajipaka mafuta ya oili chafu ili wakishikwa usiku wateleze, lakini tunakuomba Mungu ukaondoe roho chafu ndani yao ili huyo teleza atoweke na asirudi tena kuwatesa wananchi hasa wanawake wa hapa Kigoma.” alisema Baba mtakatifu.

Katika kuhakikisha wanafikisha maombi kwa hisia, aliomba waumini wote waliokusanyika katika ibada hiyo kulala chini wakiwa wamenyosha mikono na miguu kwa takribani dakika tatu kumuomba Mungu ateketeze pepo la wanaume Teleza mjini Kigoma.

Awali kabla ya maombi hayo, Anga aliyealikwa kuwa mgeni rasmi katika salamu zake aliomba kanisa lifanye maombi kulaani vitendo vya wanaume Teleza.

Ibada hii inajumuisha watu kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo (DRC), Msumbiji na Ujerumani ambapo pia imejumuisha waumini wa kanisa hilo kutoka mikoa yote nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz