Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

“Wanaume msiwakimbie watoto wenye vichwa vikubwa, mgongo wazi”

Vichwa Vikubwa Uzinduzi wa Kituo cha kulelea watoto wenye vichwa vikubwa

Sat, 12 Nov 2022 Chanzo: Mwananchi

Wazazi wa kiume wametakiwa kutowakimbia na kuwatelekeza wenza wao wanapojifungua watoto wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi huku wengi wao wakihusisha tatizo hilo na imani za kishirikina.

Wito huo umetolewa leo Novemba 12, 2022 na msimamizi wa kituo cha kulea watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi cha “Nyumba ya Matumaini Kitongo”, Getrude Laizer wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo hicho.

Kituo hicho kilichojengwa na Shirika la Child Help katika kijiji na kata ya Kitongosima, wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Laizer amesema idadi ya watoto wanaohudumiwa kituoni hapo wanalalamika kutelekezwa na waume zao baada ya kujifungua watoto hao huku akiiomba jamii kuondoa unyanyapaa dhidi ya watoto wenye changamoto hizo.

“Katika kituo chetu tunapokea watoto wanaoendelea na matibabu Bugando lakini wengi wao ukiwauliza kuhusu wezazi wao wa kiume wanasema waliwakimbia kwa sababu wanaamini matatizo haya yanasababishwa na imani za kishirikina,” amesema Laizer ambaye ni shujaa wa ugonjwa wa mgongo wazi.

Amesema pamoja na kutoa huduma kwa watoto hao bila malipo, bado wanakabiliwa na uhaba wa vitanda huku akiomba wadau na serikali kujitokeza kusaidia mahitaji hayo.

Daktari wa idara ya upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo katika hospitali ya Bugando, Dk David Sikambale amesema tatizo la mgongo wazi halisababishwi na imani za kishirikina bali ni matokeo ya upungufu wa madini ya Folic Acid kwa mwanamke wakati wa ujauzito.

Pia, amesema tatizo la kichwa kikubwa husababishwa na kichwa kujaa maji kunakotokana na maji kutuama kichwani, jambo linalopunguza ufanisi kwenye makuzi ya mtoto.

“Ndiyo maana tunawashauri wanawake kumeza dawa za Folic Acid au kula lishe bora kabla na wakati wa ujauzito ili kuwaepusha kuzaa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi. Matatizo haya hayasababishwi na imani za kishirikina,” amesema Dk Sikambale.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Child Help Tanzania, Abdulhakim Bayakub amesema shirika hilo limefanikiwa kutoa huduma na msaada kwa watoto wenye matatizo hayo zaidi ya 143.

Katika kutambua juhudi za utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto wenye matatizo hayo, Rais wa Shirika la Child Help, Pierre Mertens ametoa tuzo kwa vinara wa ulinzi wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo Laizer ameibuka mshindi wa jumla.

Wengine waliopewa tuzo hizo ni Ruth Nalugya kutoka Uganda, Phillys Migasho wa Kenya, Kipkirui wa Kenya na Ester Khamis wa Kenya.

Chanzo: Mwananchi