Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume Kigoma Tanzania wahamasika kufunga uzazi

73567 Wanaume+pic

Fri, 30 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Suala la uzazi wa mpango limeanza kuwa na mwitikio katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania, baada ya wanaume 11 katika Kituo cha afya Bitale kuamua kufunga uzazi kwa hiari yao.

Wanaume hao ni miongoni mwa watu 47 waliofunga uzazi kwenye kituo hicho kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma tangu Januari 2019 huku 36 kati yao wakiwa ni wanawake.

Hatua hiyo imefuata baada ya juhudi kuwekwa kufuatia matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi uliofanyika Kigoma mwaka 2014, kuonyesha katika viwango vya uzazi Tanzania ni watoto 5.4 kwa kila mwanamke huku Kigoma ikiwa ni watoto 6.7 kwa kila mwanamke.

Adriano Chambala (59) ni miongoni mwa wanaume walioamua kufunga uzazi baada ya kufikisha idadi ya watoto 11.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 30,2019 Chambala amesema yeye na mke wake Abia Julius (38) walitosheka na watoto waliowapata hivyo waliona njia pekee ni kufunga uzazi.

"Mke wangu wa kwanza alizaa watoto saba tukaachana, nikamuoa huyu amezaa watoto sita lakini wawili wamefariki, niliona mke anachoka shughuli ni nyingi na mimba miezi tisa lazima aende shambani ahudumie familia niliona ni heri nimpumzishe," amesema Chambala.

Pia Soma

Advertisement   ?
Chambala amefafanua kuwa hali ya kiuchumi ni sababu mojawapo inayowafanya wanaume wengi waamue kufunga uzazi, baada ya kuelimishwa umuhimu wa kufunga uzazi.

Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Nobeth Nshemase amesema mafanikio hayo yamefuatia utekelezaji wa mradi wa USAID Boresha Afya ambao umewawezesha watoa huduma kupatiwa mafunzo, upatikanaji wa vitendea kazi na dawa.

Amesema kituo hicho kinachohudumia vijiji 12 kwenye halmashauri hiyo, kimefanikiwa kutoa huduma hiyo kwa wanaume ambao wengi wao ni chini ya umri wa miaka 36.

"Huku wanaume wanaanza kuzaa wakiwa na umri wa miaka 20 na wanawake ni kuanzia 12 hadi 15, hawafuati uzazi wa mpango hivyo kila baada ya mwaka mmoja na nusu ana mimba, sasa mwanaume anapotimiza umri wa miaka 36 tayari ana watoto 10 na wapo wanazaa mpaka 14," amesema.

Katika utafiti uliofanyika mwaka 2014 ulionyesha asilimia 79 ya wanawake hawatumii njia za uzazi wa mpango, asilimia 45 walisema ni lazima wazae watoto wengi kwani wengine wanaweza kufa huku asilimia 50 wakijifungulia nyumbani.

Chanzo: mwananchi.co.tz