Moshi.Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ally, ameagiza kuongezwa kwa Faini inayotozwa kwa wakulima wa Kahawa, ambao wamekuwa wakiuza miche ya zao hilo Kinyume cha taratibu.
Ally ametoa agizo hilo leo Juni 23,2019, baada ya kupokea taarifa ya mradi wa Bustani ya Kahawa, katika Halmashauri ya Moshi Vijijini, ameelezwa kuwa miche hiyo hutolewa bure na mkulima ambaye hubainika kuiuza, hutozwa faini Sh1,300 kwa Kila mche wa kahawa.
“Mmeniambia miche hii hutolewa bure bila malipo na ikionekana mtu anaiuza kwa mtu mwingine, faini yake ni Sh.1,300,mimi ombi langu, Faini hii iongezwe, ili kuweka adhabu kali, kwa wale ambao wanauza kinyume cha utaratibu,” amesema Ally.
Aidha amesema, Halmashauri hutumia fedha nyingi kuhakikisha wakulima wanapata miche bora ya Kahawa, hivyo ni lazima wale ambao wanaiuza kwa maslahi yao wapatiwe adhabu kali.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Kahawa Wilaya ya Moshi, Violeth Kisanga, amesema halmashauri imezalisha miche 38,000 ambayo inatosha hekari 72, kwa mbegu za kahawa aina ya Compact.
Pia Soma
- Chuo Kikuu cha Addis Ababa kuanza kufundisha Kiswahili
- VIDEO: Bashe afunguka kuikosoa Serikali ya Tanzania, amtaja Lowassa
- TAWA yatangaza mkakati kuwalinda Flamingo wa Ziwa Natron