Arusha. Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Abdalah Ulega amewaonya wafugaji wenye tabia ya kutorosha mifugo na kuipeleka nje ya nchi kuacha mara na atakayekamatwa, atashtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 13, 2019 wakati akizungumza katika ufungaji wa semina ya uuzaji wa ng'ombe kwa kutumia mizani, iliyowashirikisha wafanyabiashara , wafugaji na wenyeviti wa vijiji. Semina hiyo imefanyika katika mpaka wa Namanga.
Ulega amesema wafugaji wengi wana tabia ya kutorosha mifugo nje ya nchi kwa kisingizio cha soko.
Amewataka kuuza mifugo hiyo nchini kwa sababu hivi sasa mifugo yote inapimwa kwa kilo, haikadiriwi kama ilivyokuwa awali.
Amesema wafugaji wengi hupeleka mifugo yao nje ya nchi kutokana na uhakika wa soko kwa madai kuwa huko hununuliwa kwa kilo badala ya kukadiria.
“Mfugaji yeyote atakayepatikana akisafirisha mifugo nje ya nchi atashtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi na atapelekwa jela na hatajua atatoka lini, hivyo nawaomba mfuate sheria na taratibu za nchi,” amesema Ulega.
Pia Soma
- Mwanafunzi auawa na mamba akioga Ziwa Victoria
- ANTI BETTIE: Mchumba asiyekupenda achana naye, tafuta atakayekupenda
- USHAURI WA DAKTARI: Hizi hapa sababu za wanaume kuwa na sauti nyembamba
Amesema uwapo wa mnada huo utawezesha wafugaji kupeleka mifugo yao ambayo itakuwa ikipimwa kwa kilo badala ya kukadiria na tayari mizani zimeshaletwa kwenye eneo hilo.
“Kwa kufanya hivi, wafugaji sasa watanufaika kwa kuuza bei halisi na halali itakayowapatia faida,” amesema mkurugenzi huyo.
Mhina amesema mnada huo unapokea ng'ombe 300 kwa siku na mbuzi 2,000, na biashara ya kununua na kuuza mifugo katika eneo hilo tayari ilishaanza.
Amesema changamoto bado ipo kwenye elimu jinsi ya kutumia mizani hiyo kwa wafugaji na wafanyabiashara ambayo amesema inaendelea kutolewa.
Mmoja wa wafugaji, Olesiada Sadala amesema semina hiyo imewasaidia kujua matumizi sahihi ya mizani na umuhimu wa kufuata sheria na kanuni kama kulipa kodi.
Amesema kuanzishwa kwa mnada huo wa mifugo pia kutasaidia kuondosha tatizo la kutorosha mifugo.