Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaosoma mbali wasaidiwa baiskeli

CkfwOHNUUAAGSKh Wanaosoma mbali wasaidiwa baiskeli

Thu, 29 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAFUNZI wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma waliokuwa wakitembea umbali wa kilomita sita kwenda shuleni wamepatiwa msaada wa baiskeli 52 na Shirika la Compassion International Tanzania.

Msaada huo umetolewa ili kuwasaidia wanafunzi hao kufika shuleni na kurudi nyumbani kwa kutumia usafiri huo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Mtoto AICT Pahi, Cosmas Rocket alisema hayo juzi kwenye hafla fupi ya kukabidhi msaada huo wenye thamani ya Sh milioni saba.

Hafla hiyo ilikwenda sambamba na kumuaga Askofu Mstaafu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Pwani, Charles Salala. Rocket alisema baiskeli hizo zitasaidia wanafunzi hao kufanya vizuri kitaaluma na kuondokana na vishawishi vinavyokatisha ndoto zao.

Alisema kutokana na wanafunzi wengi kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita sita kwenda shule na kurudi nyumbani kila siku, waliandaa andiko la kuomba msaada huo kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao.

“Msaada huu wa baiskeli unatoka shirika la Compassion International Tanzania, utawasaidia watoto ambao wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule ili kuwapunguzia uchovu wa safari,” alisema. Rocket alisema pamoja na msaada huo wa baiskeli, pia watoto kutoka kaya zenye mahitaji ya malazi wamepatiwa magodoro 15 ambayo kila moja limegharimu Sh 150,000.

Mary Masala kutoka kitengo cha huduma ya mama na mtoto akisoma risala ya kituo hicho cha AICT Pahi, alisema pamoja na mafanikio mbalimbali wanakabiliwa na uchakavu wa mabweni katika Shule ya Wasichana Tana.

“Pia tunakabiliwa na tatizo la uhaba wa madarasa kwa ajili ya watoto wa madarasa ya chekechea na huduma ya mtoto siku ya Jumamosi japo kanisa limejitahidi kujenga vyumba vya madarasa mawili ambayo hayajakamilika,” alisema Masala.

Mwezeshaji Kanda ya Kati wa shirika hilo, Modesta Luvanda aliwataka wazazi wa wanafunzi wilayani Kondoa kuacha tabia ya kuwalazimisha watoto wao kufanya vibaya katika mitihani ya mwisho ili wawaoze au kuwatumikisha katika kazi nyingine.

Askofu mstaafu wa kanisa hilo, Charles Salala alisema ipo haja ya jamii kubadili mitizamo yao ili kufikia maendeleo ya kweli.

“Maendeleo ya kweli yanaletwa na Watanzania wenyewe na si kutegemea misaada kutoka mataifa mengine,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz