Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaopisha bwawa la Farkwa watulizwa

66c906ca5b037d9d50ec592ccc876928 Wanaopisha bwawa la Farkwa watulizwa

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANANCHI wa vijiji vya Bubutole na Mombose, ambao wamepisha mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, wametakiwa kuwa na subira wakati malalamiko yao yakishughulikiwa.

Kauli hiyo ïlitolewa juzi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba alipokutana na wananchi hao, kujadili utekelezaji wa mradi wa bwawa hilo na kushughulikia malalamiko ya wastahiki kuhusiana na fidia.

Alisema mpaka sasa jumla ya malalamiko ya wastahiki zaidi ya 400 yamewasilishwa na yanafanyiwa kazi.

"Moja ya hoja zilizowasilishwa ilikuwa baadhi yenu hamkuwa mnaonekana kwenye jedwali la fidia la awali na wengine malipo yenu yalikuwa pungufu. Hoja hizi zote zimeshughulikiwa na jedwali la nyongeza la fidia limeandaliwa," alisema Kemikimba.

Alisema serikali itahakikisha imewalipa wananchi wote waliolipwa pungufu na ambao hawakuwepo katika jedwali la awali la kulipwa fidia, ili kila mwananchi apate haki yake inayostahili.

Tathmini ya mali za wastahiki ilifanyika na jumla ya Sh bilioni 7.7 zilitengwa kulipa fidia kwa wananchi, wanaopisha eneo la ujenzi wa bwawa hilo la Farkwa. Wastahiki 2,769, kati ya 2,868, wamelipwa sawa na asilimia 96.5 ya malipo yote. Mpaka sasa fedha zilizobaki ni Sh milioni 213.7 kwa ajili ya wastahiki 100 ambao hawajalipwa.

Ziara ya Naibu Katibu Mkuu ilifanyika baada ya ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoifanya katika vijiji vya Bubutole na Mombose Novemba 21, mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, Majaliwa aliwahakikishia wananchi kwamba hawatahamishwa mpaka miundombinu ya huduma za kijamii katika sehemu wanakohamia kukamilika.

Chanzo: habarileo.co.tz