Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaoegesha magari barabarani faini Sh200,000

21317 Miradi+pic TanzaniaWeb

Tue, 9 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakala wa Barabara (Tanroads) imeanza kutoza faini ya Sh200,000 kwa kila mtu atakayekutwa na kosa la kuegesha gari barabarani na kusababisha usalama kwa watumiaji.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 7, 2018 na Meneja wa Tanroads Dar es Salaam, Julius Ndyamukama wakati akijibu malalamiko ya Stanley Kimaro aliyekuwa akilalamikia utaratibu huo baada ya kuamriwa kulipa faini hiyo.

Ndyamukama amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiweka vyombo vyao vya usafiri katika miundombinu ya barabara bila kujali kuwa wanaweza kuhatarisha usalama kwa watumiaji.

“Kuna watu wananunua magari hawajui wapi kwa kuyalaza na badala yake wanayaacha barabarani, mwingine anapaki gari barabarani au pembezoni na kuliacha muda mrefu bila kujali usumbufu anaosababisha,” amesema Ndyamukama.

“Ndiyo maana  tumekuwa tukiwatoza Sh200,000 kama fundisho baada ya kubeba magari yao na kuyapeleka katika ofisi zetu na hela ya ‘break down’ magari maalum ya kuvuta wanalipia wao wenyewe baada ya kufanya makubaliano,” ameongeza.

Akifafanua hilo Ndyamukama amesema magari yanayotozwa faini ni yale yatakayokaa katika eneo la barabara kwa muda mrefu na haitawahusu wale wanaopaki kwa sekunde chache

Awali Stanley Kimaro aliilalamikia Tanroads kwa kubeba gari yake aina ya ‘pick up town hiace’ ikiwa ni dakika sita baada ya kuipaki na kuamriwa kulipa Sh350,000 yaani faini Sh200,000 na break down Sh150,000.

“Na nilipowaona nilibishana nao sana nikijaribu kuwaelewesha lakini walikataa na kuniambia niwafuate ofisini ambako niliamriwa kulipa pesa hiyo,” amesema Kimaro.

Chanzo: mwananchi.co.tz