Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaodaiwa kupandisha bei ya ‘sanitizer’ wabanwa

100078 Sanitizer+pic Wanaodaiwa kupandisha bei ya ‘sanitizer’ wabanwa

Thu, 26 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi amesema atawasamehe wafanyabiashara waliokamatwa kwa kosa la kuongeza bei za visafisha mikono ‘sanitizer’ endapo bidhaa hizo watazigawa kwa watoto yatima.

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Katambi alisema mbali na kuwapa ‘sanitizer’ watoto yatima pia wawape wenye ukoma waliopo Kituo cha Hombolo.

Mwishoni mwa wiki wafanyabiashara wawili wa maduka ya dawa walikamatwa kwa madai ya kupandisha bei za ‘sanitizer’ kutoka Sh3,000 hadi Sh20,000.

Hadi jana wafanyabiashara hao walikuwa wamepewa sharti la kuripoti polisi kila siku asubuhi na taarifa zimfikie mkuu wa wilaya hiyo.

“Niliwakamata kwa kutumia mamlaka ya kiutendaji, licha ya kuniomba msamaha lakini bado ninaweza kuwa na mamlaka ya kusamehe kama binadamu, lakini mpaka watakaponihakikishia ushirikiano wa kutosha na kunisaidia watoto wangu yatima na wenye ukoma ambao Serikali inapaswa kuwasaidia,” alisema Katambi.

Akizungumza na wamiliki wa maduka ya dawa baridi mwishoni mwa wiki alisema kuna watu wamepandisha bei mara kumi ya bei ya kawaida, jambo lililomkera na kuanza kuwakamata baada ya kujiridhisha wanakiuka sheria.

Pia Soma

Advertisement
Katambi alisema kazi ya kuangalia gharama za vifaa katika maduka itakuwa endelevu na atafanya kazi hiyo usiku na mchana kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Ofisa Afya wa Jiji la Dodoma, Goodluck Magoti alisema Kituo cha Afya cha Mkonze kimetengwa kwa ajili ya dharura kama watakuwa na mgonjwa au mtu wanaemhisi ana dalili za corona.

Magoti alisema wameweka utaratibu katika maeneo ya jiji ambayo yanakuwa na mikusanyiko, lazima kuwapo na vyombo vyenye majisafi ya kunawa na sabuni.

Pia, alisema wenye uwezo wa kununua dawa ya kusafishia mikono wameelekezwa wanaweza kutumia majisafi na sabuni.

Chanzo: mwananchi.co.tz