Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashim Komba amewaagiza madalali wa magari katika eneo la Uwanja wa Sigara uliopo Sinza B wilayani humo kuacha kutumia eneo hilo la wazi kwa ajili ya kupaki na kuuzia magari na kupisha eneo hilo kuwa wazi kama lilivyotengwa na Serikali.
DC Komba ametoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya wananchi wa eneo hilo la kutaka eneo libaki wazi kama ilivyokua awali huku wakimuomba kuagiza kubomolewa kwa ofisi ya CCM inayojengwa ndani ya eneo hilo la wazi.
Aidha, DC Komba amesema eneo la Sinza B lina changamoto ya kuvamiwa kwa maeneo ya wazi, ambapo takribani maeneo 61 yamevamiwa na nyumba kujengwa hivyo zoezi la kusafisha maeneo ya wazi linaweza kuathiri watu wengi na halitakiwi kufanywa kwa kubagua, na hata hivyo CCM imekodishwa eneo hilo kwa masharti ya kuondoa miundombinu yoyote watakayoiweka kwa gharama zao, pindi serikali itakapohitaji eneo lake, na kuuagiza uongozi wa Chama cha Mapinduzi Kata Sinza, kuhakikisha wanatekeleza sharti hilo kwa mujibu wa makubaliano.
Akizungumza kuhusu mgogoro huo, Diwani wa Kata ya Sinza, Raphael Nyange amesema CCM inajenga eneo hilo kwa kufuata taratibu na kuwa ujenzi huo umeendelea huku wakazi hao wakiona na hakuna ujenzi unaofanywa usiku kwa usiku na kwa kificho kama ambavyo imekuwa ikielezwa.