Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi watakiwa kuiunga mkono Serikali ili kukamilisha miradi

DSC 3356 Wananchi watakiwa kuiunga mkono Serikali ili kukamilisha miradi

Sat, 5 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wa Wilaya ya Kalambo wametakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha miradi ya maendeleo ikiwemo zahanati na vituo vya afya vinakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ametoa wito huo ( Novemba 04,2022) wakati alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Oktoba 20 mwaka huu kwa uongozi wa Wilaya ya Kalambo kuhakisha miradi ya afya ya zamani inatengewa fedha na kukamilishwa.

“Nimepita kuja kujionea hali ya utekelezaji wa maalekezo yangu ambapo nimeona tayari halmashauri imeanza kutoa fedha na kazi za kukamilisha zahanati ya kijiji cha Kapozwa, kituo cha Afya Kanyezi na Legeza mwendo zimeanza” alisema Sendiga.

Sendiga aliongeza kusema ziara zake kwenye halmashauri zinaendelea ili kuhakikisha Rukwa inaondokana na uwepo wa miradi viporo hususan kwenye sekta ya afya.

“Nawataka watendaji wote wa serikali kwenye mkoa huu wawajibike ili kuleta matokeo chanya kwa kutatua changamoto za miradi ya maendeleo. Nitahakikisha ninafika maeneo yote kuwatatulia kero wananchi na kuwa hakuna changamoto katika utendaji tutashindwa kuitatua” alisisitiza Sendiga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Shafii Mpenda akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Kapozwa alisema ataendelea kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo miradi iliyotolewa maelekezo na Mkuu wa Mkoa Sendiga.

Shafii aliongeza kusema nguvu za wananchi zilizotumika kutekeleza miradi ya afya itaenziwa kwa halmashauri kutoa fedha kukamilisha miradi hiyo ambapo ametoa wito kwa wananchi kutochoka kuchangia nguvu zao.

Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa Sendiga amekagua ujenzi wa kituo cha Afya Mwazye ambacho ameagiza kianze kutoa huduma mwisho wa mwezi huu Novemba huku kituo cha Afya Kanyezi kimepatiwa shilingi Milioni Arobaini na Kituo cha afya Legeza Mwendo kimepatiwa shilingi Milioni Sitini ili vikalimishwe kabla ya Desemba mwaka huu .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live