Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wataka utatuzi kero ya maji Handeni

Fsrest Wananchi wataka utatuzi kero ya maji Handeni

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Wananchi wa Kata ya Kwediyamba Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga, wamemuomba Mbunge wa jimbo hilo, (CCM) Reuben Kwagilwa kuwasaidia kukamilisha mradi wa maji uliopo kwenye eneo hilo kukamilika, ili kuondokana na shida ya maji inayowakabili.

Wakizungumza wakati wa ziara ya mbunge huyo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye jimbo hilo jana Aprili 5, 2024, wananchi hao wamesema kwa sasa hawana huduma ya uhakika ya maji, hivyo endapo mradi uliopo kwenye kata yao ukikamilika utaondoa shida hiyo.

Mkazi wa kata ya Kwediyamba, Fatuma Mwilo amesema eneo hilo lina shida kubwa ya maji, ambapo wananchi wanalazimika kukesha kwenye visima kutafuta maji, hivyo mradi huo ukikamilika utakuwa ni mkombozi kwao na wataepukana na tatizo hilo.

Amesema kuwa kwa sasa wanatumia maji ya visima vya asili na mvua lakini vyanzo hivyo maji yake sio salama.

Akizungumza na wananchi hao Kwagilwa amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh1.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata hiyo, ili kutatua tatizo la kukosekana huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.

Amesema ndani ya siku 30 mpaka 60 kuanzia sasa mradi utakuwa umekamilika na wananchi wataanza kupata huduma ya maji, hivyo atakwenda kuhimiza wizara ya maji kutoa kiasi cha fedha kilichobaki ili mkandarasi amalizie mradi huo.

Fundi sanifu kutoka Mamlaka ya Maji ya Handeni Trunk Main (HTM), Ali Shemahonge amesema mradi huo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 63 na inahitajika Sh478 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na umaliziaji.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni, Amiri Changogo amewataka wataalamu wanaosimamia mradi huo, kuhakikisha unajengwa kwenye viwango vinavyolingana na thamani ya fedha iliyotolewa..

Chanzo: Mwananchi