Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango, amemuelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo, kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu fursa zilizopo katika biashara ya hewa ya ukaa.
Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Katuma Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, mara baada ya kukabidhi hundi ya Sh bilioni 2.3 kwa wananchi wa vijiji 8 vya Wilaya hiyo, iliyotokana na mauzo ya mradi wa hewa ya ukaa.
"Kwa sasa mataifa yaliyojikita katika biashara hii yanatumia soko huria kutokana na ugumu wa mikataba inayoendana na soko la kimataifa, kumekuwa na kampuni binafsi, ambazo zinajikita katika biashara hii ya hewa ya ukaa," alisema.
Amesema wizara ihakikishe upungufu wote wa kisera na usimamizi wa biashara ya hewa ya ukaa unapatiwa ufumbuzi, ili taifa liweze kunufaika na biashara hiyo.
Dk. Mpango ameipongeza taasisi ya Carbon Tanzania, kwa kushirikiana na taasisi ya Tuungane Tanzania chini ya mradi uitwao Ntakata-Mountains Redd Pluss Project, kwa kufadhili mradi huo na amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo,Frank Kweka, ambaye ni Meneja wa mradi wa hewa ukaa Ntakata, amesema mradi huo ulianza mwaka 2018.
Amesema katika awamu ya tano tokea kuanzishwa kwake wananchi wa vijiji hivyo wapatao 34,000 wamekatiwa bima za afya, kupeleka vyakula shuleni, ujenzi wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya ikiwemo kutoa ajira.
Kweka amesema, mradi wa hewa ukaa unalenga kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na misitu kwa kuhakikisha hawaichomi moto, kukata miti na kufanya shughuli nyingine hatarishi kwa uhifadhi wa misitu, badala yake wananchi wahamasike kupanda miti katika maeneo yao.
Kupitia mradi huo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika inapata asilimia 10 ya fedha zinazopatikana baada ya mauzo ya hewa ya ukaa, ili kugharamia shughuli za usimamizi, wakati asilimia 90 zinagawiwa kwenye vijiji vilivyo katika mradi wa msitu wa Tongwe Magharibi, unaokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 230.