Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi waonywa kuuza ardhi kiholela kwa wageni

IMG 20221113 WA0283 Wananchi waonywa kuuza ardhi kiholela kwa wageni

Wed, 16 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi na viongozi wa Vijiji vya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wameonywa kutouza ardhi kiholela kwa wageni kwani miaka ijayo watajuta kwa kukosa ardhi kwani ardhi haiongezeki ila watu wanaongezeka.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer ameyasema hayo kwenye tafrija iliyofanyika nyumbani kwake Kata ya Naisinyai baada ya kumshukuru Mungu katika Kanisa la KKKT kutokana na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo hivi karibuni.

Amesema hivi sasa Wilayani Simanjiro kumezuka wimbi la wananchi na viongozi wa baadhi ya vijiji kuuza ardhi kwa watu wanaotoka wilaya za jirani bila kutambua kuwa huo ndiyo urithi wao.

Amesema wananchi hao wakiuza ardhi yao miaka ijayo watakuja kuwa mizigo kwani watalalamika kwa viongozi kuwa hawana ardhi ili hali walishakuwa na ardhi kisha wakaiuza.

“Kila wakati nitakuwa ninakemea hili suala la uuzaji wa ardhi kwani watu wanakuja kutoka wilaya na mikoa jirani na kununua ardhi kwa bei chee Simanjiro ili hali huo ndiyo urithi wa wana Simanjiro,” amesema Kiria.

"Mtawaachia nini watoto wenu, ardhi inanunuliwa na wageni, hakuna siku utanunua ardhi tena hiyo ardhi kwa wageni, ardhi haiongezeki, kwa kiongozi wa serikali hakuna Mwenyekiti mwenye mamlaka ya kutoa ardhi bila idhini ya mkutano mkuu wa Kijiji," amesema Kiria.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Hassan Serera, akizungumza kwenye tafrija hiyo amewataka wananchi na viongozi wa Simanjiro kuwa na uzalendo na Simanjiro yao.

"Ninyi wenyeji ndiyo watoto wa chumbani hivyo mnapaswa kuwa na uzalendo na uchungu zaidi na maendeleo ya Simanjiro kuliko sisi viongozi wa kuteuliwa ambao ni watoto wa sebuleni," amesema Dkt Serera.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live