Mwanza. Diwani wa Ibungilo, Yusuf Msoke na Mwenyekiti wa mtaa wa Kiloleli A, Edgeni Lutahiwa wamedai Musa Ally (25), aliyejirusha juzi katika jengo la Rocky City Mall jijini Mwanza na kufariki dunia si mkazi wa Kiloleni.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Desemba 22, 2018, Msoke amesema wananchi wa kata ya Ibungilo wanafahamika na iwapo kama kijana huyo angekuwa mkazi wa Kiloleni kama walivyoeleza polisi, wangekuwa wanamfahamu.
Jana Ijumaa Desemba 21, 2018 kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Advera Bulimba amesema kijana huyo alionekana akiwa amelewa kupita kiasi na tangu Desemba 16, 2018 na alikamatwa na kuwekwa kituo cha polisi Kirumba, kilevi kilipopungua aliachiwa.
Bulimba amesema baada ya polisi kumuachia alikwenda kunywa tena pombe na baadaye kujirusha kutoka ghorofa ya tatu na kukutwa na pombe kali na ugoro
Katika ufafanuzi wake Msoke amesema ana mashaka ya majina yaliyotumika kumtambulisha marehemu, kwamba iweje msiba hata usijulikane uko wapi.
“Huyu kwa kweli sio wa hapa. Watu wangu wote wana utaratibu wa kutambuana katika daftari maalum la 'wananzengo'. Kama ni wa hapa itafahamika tu hata kama sio leo," alisema Msoke.
Kwa upande wake Lutahiwa amesema hajawahi kusikia jina la marehemu.
“Mimi niliona tu mitandaoni kuna mtu kajirusha kutoka ghorofani na baadaye ikaelezwa kuwa ni mkazi wa hapa, pengine ndugu zake wanaogopa kujitokeza,” alisema.
Justine Madereke, mkazi wa mtaa huo amesema hakumtambua marehemu huyo, “Huwa (marehemu) anazunguka hapa sokoni muda wa mchana na anakuwa ni mlevi tu. Sasa kwa kuwa sisi hatumfahamu hatukuwa na nia wala haja ya kumdadisi.”
Katika maelezo yake Bulimba alisema wakati polisi wakimhoji marehemu alidai ni mhitimu wa Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu Dar es Salaam, kulalamika kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kukosa kazi.
“Marehemu alidai kuwa ni msomi, hana kazi na pia ni yatima. Wakati jeshi la polisi wakichukua maiti hiyo ilikuwa na kijikaratasi kimeandikwa kwamba asilaumiwe mtu," alisema Bulimba.
Soma Zaidi: Msomi UDSM ajirusha ghorofani, afariki dunia