Wananchi wa kijiji cha Seke Ididi kata ya Seke Bugolo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wameiomba Serikali kuwajengea zahanati ya kijiji hicho iliyobomolewa kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
Ombi hilo limekuja baada ya zahanati yao waliyoijenga na kufika hatua ya lenta kwa kutumia fedha walizochangishana kubomolewa kisha kujengwa ofisi za kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) inayotekeleza mradi wa SGR.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea katika kijiji hicho leo Jumanne Agosti 22, 2023 wamesema wanapata changamoto wanapohitaji matibabu hasa watoto wadogo na wajawazito wanapohitaji huduma ya kujifungua kutokana na umbali wa kilomita saba wanapotakiwa kufuata tiba.
“Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutuletea mradi huu wa reli ya mwendo kasi, lakini tunaiomba itusaidie kutujengea zahanati yetu iliyobomolewa kwani tuliona kuna changamoto kubwa ndiyo maana tukaamua kuchangishana ili tuwe nayo karibu na baada ya kampuni hii kuomba ijengwe hapa tuliahidiwa tutajengewa sehemu nyingine zahanati hii na tulipewa kiwanja kabisa,
“Lakini mpaka sasa mradi huu unaelekea mwishoni hatujajengewa tunaona tu wenzetu wanaendelea na kazi zao, hivyo tunaona kama vile tumesahaulika kabisa ukiangalia na watu wameshakuwa wengi katika kijiji hiki lakini hakuna hata zahanati, tunaomba mama yetu, Rais Samia utuhurumie tunateseka…tujengewe zahanati yetu iliyobomolewa,”amesema Phinius Mauma
Mkazi wa Kijiji cha Seke Ididi, Adija Makongolo amesema wanawake wanapata changamoto sana pale wanapoumwa uchungu na muda mwingine wanajifungulia njiani.
Mwenyekiti wa kijiji cha Seke mjini, Omary Abdalah amesema kutokana na ujenzi wa SGR watu wamekuwa wengi wanaohitaji huduma za afya, lakini hazipo hapo nakuwafanya wananchi wakimbilie kata za jirani kupata tiba.
“Sisi tulikuwa tumepata eneo letu na mabati yalikuwa tayari yameandaliwa na hospitali ingekuwa imeshaanza kutumika lakini sasa kimya tunashindwa kuelewa ni kwa nini hatujengewi na huku tuliahidiwa kwamba tunajengewa,”amehoji Abdalah
Diwani wa Kata ya Seke Bugolo, Ferdnand Mpogomi amesema kutokana na wananchi kuchoka kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya kata jirani waliamua kuchangishana fedha zao kuanzisha ujenzi huku, mfuko wa jimbo ukitoa mifuko 75 ya saruji kujenga zahanati iliyobomolewa.
Amesema baada ya kuanzishwa mradi huo uthaminishaji ulifanywa na kuonekana inatakiwa kulipwa fidia ya Sh10 milioni huku wananchi wakitoa eneo la hekari tatu, kutafuta mzabuni pamoja na kusomba mchanga lakini hawaoni kinachoendelea.
“Tayari tulitafuta mzabuni ambaye alikuwa ameleta hadi vifaa vyake kwa ajili ya kuanza ujenzi lakini baada ya kuona kimya alibeba vifaa vyake na kwenda kufanya kazi sehemu nyingine, tunaomba tujengewe zahanati kwani inaonekana fedha hizi zimepotea. Tunamuomba Rais na Waziri wasikilize kilio chetu, vijiji nane viko bega kwa bega na Rais,”amesema Mpogomi
Amesema pia kisima cha maji kijiji cha Dulisi kinachotegemewa na wananchi kimepitiwa na mradi huo, waliambiwa mkandarasi atawajengea kingine lakini mpaka sasa bado hajajenga na wananchi wa kijiji hicho wamebaki wakiteseka kutafuta maji.
Meneja wa SGR kituo cha malampaka, Christopher Lamshai amesema mpaka sasa hakuna taasisi ya Serikali ambayo imeshalipwa na maelekezo ni kila mkurugenzi wa halmashauri husika awasiliane na Katibu Mkuu wake ili waingie kwenye mchakato wa kujenga kwani kuna taasisi mbalimbali za kiserikali ambazo zimepitiwa na mradi lakini bado hazijalipwa.
“Hivyo tutaendelea kuikumbusha wizara ili iweze kuwatekelezea mahitaji yenu ya zahanati, lakini lile la kisima hilo nitalifuatilia mimi mwenyewe ili kujua tunafanya utaratibu gani wananchi waweze kuchimbiwa kisima sehemu nyingine,”amesema Lamshai