Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi walalamikia mazoezi ya utayari, TAA yawaomba radhi

AJALI MSDF Wananchi walalamikia mazoezi ya utayari, TAA yawaomba radhi

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ikikanusha taarifa za uwepo wa ajali ya ndege ndani ya Ziwa Victoria kwa kile ilichodai ni zoezi la utayari, wakazi wa mkoa wa Mwanza wamesema mazoezi hayo yamewaachia mshtuko.

Wananchi wametoa kauli hiyo jana Alhamisi Februari 23, 2023 wakiwa kwenye mwambao wa Ziwa Victoria ambapo zoezi la utayari wa majanga linalodaiwa kutekelezwa na Mamlaka ya Uwanja wa ndege mkoa wa Mwanza lilipotekelezwa.

Mkazi wa Ilemela mkoani Mwanza, Tula Andrea amesema taarifa ya ajali ya ndege kuzama ndani ya Ziwa Victoria imemshtua jambo lililomlazimu kwenda eneo ilipodaiwa kutokea na kukuta hakuna majeruhi wala watu waliodhurika huku akidai anarejea nyumbani huku akiwa haelewi kilichotokea.

"Nimesikia mitandaoni kwamba kuna ajali imetokea, nimeshtuka sana ikanibidi nikimbie hadi huku ziwani ambako ajali imedaiwa kutokea lakini sijaikuta hiyo ajali badala yake watu wanasema yalikuwa mazoezi ya utayari, ninaondoka lakini bado sijaelewa kinachoendelea," amesena Tula.

Prisca Magabe ambaye ni Mkazi wa Kiloleli wilayani Ilemela mkoani Mwanza amesema taarifa ya ajali ya ndege hiyo inayodaiwa kuwa ni mazoezi ya utayari mbali na kuzua taharuki, pia itajenga taswira kwa jamii kupuuza hata utakapotokea ajali halisi wakidhani ni mazoezi ya utayari.

"Kuna watu wana ndugu zao walikuwa wanasafiri na ndege za leo asubuhi kwa hiyo kama wamesikia taarifa ya uwepo wa ajali ya ndege lazima wamepata mshtuko, wengine wataathirika kisaikolojia nafikiri hii tabia siyo nzuri kwa afya zetu," amesema

Hata hivyo, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Seneth Lyatuu ameieleza Mwananchi Digital leo kuwa mazoezi hayo ya utayari yanafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Anga ya mwaka 2006 na kanuni za uendeshaji wa viwanja ya mwaka 1974 Na kiambata cha 14 cha Shirika la Usafiri wa Anga duniani.

Lyatuu amesema sheria hizo zinazitaka mamlaka za usafiri wa anga kufanya majaribio ya utayari wa kukabiliana na majanga yanapotokea huku akiomba radhi wananchi waliopata athari kutokana na mazoezi hayo.

"Tunawaomba radhi wananchi ambao wamepatwa na mshtuko kutokana na mazoezi haya, lakini utaratibu unatuhitaji kufanya mazoezi haya ya kushtukiza ili kupima utayari kwa mamlaka zinazohusika na majanga wakiwemo watoa huduma za afya iwapo wako tayari kukabiliana na majanga yanapotokea.

"Hata mashirika ya ndege ya kimataifa yakiona utayari huu yanavutiwa kuleta ndege zao zitue kwenye uwanja wetu kwa maana watakuwa wanaelewa kwamba hata ikitokea hitilafu upo uwezekano wa watu kuokolewa," amesema Lyatuu.

Zoezi hilo la utayari ni mwendelezo wa kipimo cha utayari kwa vyombo na mamlaka za uokozi ambapo Februari 13, mwaka huu baada ya ndege kudaiwa kudondoka katika uwanja wa ndege wa Kahama mkoani Shinyanga na kuzua taharuki kwa Umma ambapo baadae ilikanushwa na kubainika ni mazoezi ya utayari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live