Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi walala stendi Moshi, magari binafsi yapakia abiria

34764 Pic+stend Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wenye magari binafsi kupakia abiria na wasafiri waliokosa usafiri kuhofia kupoteza ajira, ni baadhi ya mambo yaliyojitokeza jana asubuhi katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi kutokana na shida ya usafiri iliyotokana na mabasi mengi kujaa na hivyo watu wengi kukwama kusafiri.

Mwananchi lilipiga kambi katika stendi hiyo kuanzia saa 11 alfajiri na kushuhudia idadi kubwa ya wasafiri wakihaha huku magari binafsi yakipakia abiria kwa Sh35,000 kwenda Dar es Salaam, lakini baadhi yakiwataka kushukia Chalinze mkoani Pwani.

Kwa waliokuwa na upungufu wa nauli walikosa usafiri na miongoni mwao walieleza hofu yao ya kupoteza ajira zao.

Baadhi ya abiria waliamua kurejea majumbani na wengine kuendelea kuwepo katika eneo hilo wakiwa na imani ya kupata usafiri utakaowafikisha wanakokwenda.

Miongoni mwa waliokuwa wakisotea usafiri ni Joseph Kiluwa ambaye ni mgonjwa aliyekuwa akisafiri kwenda Dar es Salaam kutibiwa.

Kiluwa alilionyesha Mwananchi vidonda mwilini akizungumzia ugumu wa safari yake kwenda jijini humo alikoitwa na wanawe kutibiwa.

“Nimefika hapa tangu saa 12:30 asubuhi. Mimi ni mgonjwa na sasa hivi (jana) ni saa tatu asubuhi naelezwa usafiri hakuna. Kwa kweli nauli imekuwa kubwa sana, hivi sisi wakulima tutasafiri kweli?” alihoji.

“Wakatisha tiketi wanasema nauli ni Sh40,000 hadi Sh50,000 na wakishasema hivyo hawageuki hata nyuma, abiria akitoa kiasi hicho cha fedha anapata usafiri na kutakiwa kutunza siri.”

Ashura Jumanne alisema Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeshindwa kuwa na mkakati mzuri kuhakikisha shida ya usafiri inamalizika.

“Jana (juzi) nimelala hapa stendi ili niwahi magari ya saa 11:00 alfajiri, ila cha kushangaza mabasi yote yakija yamejaa na si makubwa wala madogo. Mie ni mgonjwa na kesho (leo) natakiwa niwe Muhimbili (Hospitali ya Taifa) lakini usafiri hakuna,” alisema.

Johnson Mmari alisema, “Nimetokea Arusha nimetumia gharama kubwa kufika hapa halafu naelezwa usafiri hakuna. Hapa nilipo sijui nielekee wapi kwa sababu tunauliza (usafiri) tunaelezwa kuwa kuanzia tarehe 10 ndio kuna tiketi.”

Alisema, “Wengine tunawahi kazini sasa kama hakuna usafiri italeta shida kwa mabosi wetu, sidhani kama nitaeleweka. Kama leo (jana) nikikosa usafiri nitalala hapa stendi na ikishindikana zaidi nitalazimika kupanda Fuso.”

Kwa upande wake, Agnes Tesha aliyekuwa akitafuta usafiri kuelekea Morogoro aliitupia lawama Sumatra akisema imeshindwa kudhibiti kupanda kwa nauli kutoka Sh28,000 hadi Sh50,000.

Magari binafsi kicheko

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi ulibaini kuwa magari binafsi yalitumia fursa ya uhaba wa mabasi kusafirisha abiria kwa kati ya Sh35,000 hadi 45,000 kwenda Dar es Salaam. “Hii kwangu naona ni fursa maana wanasema kufa kufaana. Ukipata abiria wanne tayari una Sh140,000 na hapo nawafikisha Chalinze tu,” alisema Hassan Said aliyekuwa akipakia abiria kwenda Dar es Salaam.

Wakesha stendi

Wasafiri waliokesha katika stendi hiyo usiku wa kuamkia jana baada ya juzi kukosa usafiri walieleza mambo waliyoyashuhudia usiku.

Gaudensia Tarimo alisema usiku maduka yalifungwa na hivyo kukosa mahitaji muhimu. “Nilifika hapa na watoto wangu kwa kuwa nilikosa usafiri sikuwa na jinsi zaidi ya kulala hapa kuliko kurejea kijijini. Leo (jana mchana) nimebahatika kupata usafiri katika hii Coaster ingawa nauli ni kubwa,” alisema.

Sumatra wafafanua

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Kilimanjaro, John’s Makwale alisema: “Tunachunguza na tukiwabaini wanaopandisha nauli tutawakamata.”

Chanzo: mwananchi.co.tz