Tatizo la ukosefu miundombinu ya majengo katika Shule ya Sekondari Sanya iliyopo Kata ya Nasai wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, sasa litakuwa ni hadithi kwani Serikali imetoa Sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba saba vya madarasa na mabweni miwili kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa uchimbaji msingi kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa mabweni hayo, baadhi ya wananchi wa kata hiyo wamesema kumalizika kwa mabweni hayo kutasidia kulala kwa amani bila usumbufu.
‘’Ni kweli wanafunzi hao walikuwa wanalala katika vyumba vya madarasa kitu ambacho kiafya sio sahihi na ni usumbufu,” amesema mmoja wa wananchi hao Alex Massawe.
Massawe ambaye ni mkazi wa Koboko Kaskazini amesema wamefurahishwa na Serikali kuwapelekea mradi huo, kwani ni wa muhimu sana na kwamba kama wangejenga kwa nguvu za wananchi, basi ingechukua muda mrefu kutokana na ujenzi kuwa ghali.
‘’…tungetumia nguvu zetu katika kujenga, tungechangishana kila mwananchi labda kila Sh20, 000 pamoja na nguvu zetu pengine sizisitoshe, hivyo hatuna budi kuishukuru Serikali wangeweza kupeleka maeneo mengine,’’ amesema Massawe.
Joseph Mmar ambaye ni Mwenyekiti wa Koboko Kaskazini amesema wanafunzi hao walikuwa na changamoto ya kulala: “Kwa sasa tumeanza ujenzi huu, tutashirikiana na wananchi kuhakikisha mradi huu unaisha kwa wakati na kuanza kutumika”
Diwani wa kata hiyo Haphurehi Kifumo, amesema mbali na mabweni kukamilika pia vyumba saba vya madarasa vitakamilika na hivyo kupunguza wingi wa wanafunzi kukaa kwa kubanana na kwamba wakati mwingine kunasabasha hata ufaulu kushuka.
“Hatuna budi kushukuru Serikali kwa kutuletea fedha hizi, Tanzania ni kubwa wangeweza kupeleka sehemu nyingine lakini wametuoana sisi tunashukuru sana,” amesema.