Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi waililia Serikali kuwanusuru vipigo vya mgambo Rombo

Mgambo Askari Wananchi waililia Serikali kuwanusuru vipigo vya mgambo Rombo

Thu, 27 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Wananchi wanaoishi katika vijiji vya Kikelelwa na Motamburu, kata ya Tarakea Motamburu wilayani Rombo wanadai kupigwa na kunyang'anywa fedha na mgambo wa halmashauri kwa madai ya kupita karibu na Msitu wa Nusu Maili wakati wakienda kwenye shughuli zao za kilimo.

Wamesema wanapopita kwenda kwenye shughuli zao wanakamatwa na kupigwa bila sababu na wakati mwingine wanawekwa kwenye moja ya nyumba na kulazimika kutoa kiasi cha fedha kuanzia Sh200, 000 hadi 300,000 ndipo waachiliwe.

Wananchi hao wamesema mgambo hao wamekuwa wakiwafanyia vitendo hivyo vya ukatili kwa muda mrefu na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao licha ya kuwajeruhi.

Mkazi wa Kijiji cha Kikelelwa, Edward Tesha amesema wamekuwa wakiishi kwa tabu kutokana na manyanyaso wanayofanyiwa na mgambo hao na wakati mwingine wanahofia kwenda kwenye shughuli zao za kilimo kutokana na vichapo wanavyopewa.

"Unakuta wanaume na wanawake wanapewa vichapo kama watoto wadogo, wapo baadhi ya watu ambao wamejeruhiwa vibaya na mgambo hawa lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao," amesema Tesha.

"Tunamwomba mkuu wa wilaya aingilie kati jambo hili maana tumekuwa tukiishi kwa woga kutokana na manyanyaso tunayoyapata kutoka kwa mgambo hawa wa halmashauri, ukiangalia migongo ya watu ina alama kibao, tunataka kujua kama hawa mgambo wapo kwa mujibu wa sheria kwanini wanafanya ukatili kwa wananchi na wakati unakuta hakuna aliyevunja sheria," amesema Tesha.

"Kuna ndugu zangu walikamatwa na hawa mgambo wakapelekwa moja ya nyumba ya mtu wakafungiwa ndani na wakati tulipotaka kuwatoa wakatuambia hawawatoi mpaka kila mtu atoe Sh300, 000 huu ni ukatili usiovumilika imekuwa ni kama mradi wa mtu binafsi hii inatuumiza,"amesema Tesha

Diwani wa kata hiyo, Felichism Oisso amesema taarifa za malalamiko ya wananchi kupigwa zipo na kwamba wananchi wakiwa wanaenda kwenye shughuli zao za kilimo wamekuwa wakipigwa ovyo bila kujali wanakwenda wapi.

"Tumepokea taarifa na malalamiko ya wananchi kwa namna ambavyo wanafanyiwa vitendo vya ukatili mashambani, kuna mashamba mengine tunalima kule Msitu wa Rongai. Sasa watu wetu wanapokutana na mgambo hawa wakiwa wanaenda kwenye majukumu yao ya kila siku wanapigwa ovyo, hawataki kujua wanaenda wapi au anatoka wapi kinachoendelea ni kichapo na kunyanganywa fedha na simu,"amesema diwani huyo.

"Tunalaani kwa nguvu zote vitendo hivi vinavyofanywa na mgambo hawa na hatuko tayari kukubaliana navyo kuona watu wakipigwa, kuna baadhi ya watu wengine tumeona wana makovu kwenye miili yao baada ya kujeruhiwa na mgambo hawa," amesema.

Ameongeza "Kama mtu amefanya makosa kuna hatua anatakiwa achukuliwe na sio kupigwa kama punda hawa watu wamekuwa sio walinzi tena wamebadilika kuwa wezi na wanyang'anyi wa fedha na simu," amesema.

Alipotafutwa Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Hamis Maiga amesema malamamiko hayo ya wananchi kupigwa ameyasikia na kwamba amemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufika katika maeneo hayo kuangalia ni nini kinachoendela kuhusiana na malalamiko hayo ya wananchi.

"Haya malalamiko nimeyasikia na tayari nimemwagiza mkurugenzi aende kwenye maeneo hayo awasikilize kwasababu wanaoalalamikiwa ni watu wake,"amesema Kanali Maiga.

Chanzo: mwanachidigital