Siku chache baada ya kuripotiwa kuuawa kwa kijana Ibrahim Nicodems (22) kwa kuchomwa kisu na Thomas Amsii katika mtaa wa Sawe kata ya Maisaka mjini Babati na mtuhimiwa huyo kuachiwa kwa dhamana,wananchi wa mtaa huo wamekuja juu wakitaka haki itendeke.
Kufuatia hatua hiyo, mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amelazimika kufika Sawe na kuzungumza na wananchi hao ambao walidai kuwa hawajaridhishwa na upelelezi uliofanywa juu ya tukio hilo la mauaji.
Mkuu wa wilaya ya Babati lazaro Twange ameagiza wote waliohusika kumtoa kwa dhamana mtuhumiwa wa mauaji hayo wakamatwe na kufikishwa rumande. Mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya mauaji hayo Juni 28,2022 katika mtaa wa Sawe mkoani Manyara majira ya saa 10 jioni.
Aidha wananchi hao wamedai kuwa hawana imani na mwenyekiti wa mtaa wao Bwana Michael John kwa madai kuwa hatendi haki na hatimizi majukumu yake ipasavyo madai ambayo mwenyekiti huyo ameyakanusha.
Hata hivyo Twange aliwaongoza wananchi hao kupiga kura ya wazi ambao wengi wao 47 walisema hawamuhitaji Mwenyekiti huyo huku wengine 36 wakisema anafaa.
Pamoja na hayo Twange amesema ofisini kwake amepokea malalamiko mengi yanayomhusu Kiongozi huyo wa Mtaa na kwa kuwa kikao hicho ni cha kisheria maamuzi ya wananchi yapo sahihi.