Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wahimizwa kutoa taarifa za madhara ya dawa mapema

Fdxxg Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omary Sukari.

Wed, 15 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omary Sukari amewataka waratibu wa ufuatiliaji usalama wa dawa mkoani humo kufuatilia na kutoa taarifa za matukio ya maudhi au madhara yanayotokana na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba.

Dk Sukari ametoa wito huo leo Mei 15, 2024 wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa waratibu wa ufuatiliaji usalama wa dawa kutoka halmashauri sita za mkoa huo, yakilenga kuwajulisha namna nzuri ya utoaji taarifa ya madhara ya dawa ili mamlaka ziweze kuchukua hatua za haraka.

Amesema taarifa hizo zitaiwezesha Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kujua aina za dawa zenye changamoto na kuangalia usahihi wake, ili zisizofaa zizuiliwe mapema kabla ya kuleta madhara.

Pia, amesisitiza kwamba utoaji taarifa wa maudhi au madhara ya dawa mapema utasaidia TMDA kufanya tathmini na uamuzi kama dawa husika iendelee kuwa sokoni au iondolewe, lakini pia itasaidiwa kuwaeleza watengenezaji kuongeza ujumbe wa namna watumiaji wanaweza kuzuia madhara yatokanayo na dawa husika.

Dk Sukari amesema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa ambayo takwimu za ufuatiliaji wa matukio ya madhara au maudhi yatokanayo na dawa ziko chini zikionyesha mwaka 2022/23, malalamiko 42 pekee yaliripotiwa kati ya malalamiko zaidi ya 7,000 yalivyoripotiwa nchini, huku mwaka 2023/24 yakiripotiwa 27 pekee.

“Tunatoa dawa, vifaa tiba na chanzo kwenye vituo vyetu 247 vilivyopo kwenye mkoa huu na kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inataka wateja 200 kati ya milioni moja waliopata huduma za dawa, chanjo au vifaa tiba watolewe taarifa zao, lakini utaona kiwango kinachotolewa taarifa ni kidogo sana, hakiendani na uhalisia.

“Kusanyeni takwimu kwenye mifumo iliyopo, chambua na kuifanyia tafsiri dawa uliyotoa madhara yanawapata watu wa umri gani, baada ya hapo ikusaidie kufanya uamuzi na kutoa taarifa kwenye kituo na wadau wengine ikiwemo TMDA ambao nao watapeleka kwenye ngazi mbalimbali,” amesisitiza.

Amesema kuna uwezekano wa madhara kwa wananchi ikiwemo ulemavu hususan watoto na wengine kupoteza maisha, hivyo wajibu wao kutoa taarifa mapema ili hatua za haraka zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuondoa dawa husika sokoni.

Katika hatua nyingine, Dk Sukari amepiga marufuku uuzwaji wa dawa kwa kutembeza mitaani, kwenye magulio na maduka ya vyakula kwa kuwa kufanya hivyo kunapunguza ubora wa dawa husika.

Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi, Edger Mahundi amesema mafunzo kwa waratibu juu ya madhara yatokanayo na dawa, chanjo ni muhimu kwa sababu yamelenga kuongeza taarifa zinazotakiwa kuripotiwa kwenye mfumo wa kufuatilia usalama wa dawa nchi nzima.

“Madhara tunayozungumzia ni yale ambayo hayategemewi kutokea, mfano amepewa sindano ya Diclofenac kupunguza maumivu lakini licha ya kupewa dozi kwa usahihi, maumivu hayapungui, kwa hali hii lazima ifuatiliwe usalama wa ile dawa,” amesema Mahundi.

Amewataka wananchi wanaotumia dawa na kupata madhara kutokaa kimya na badala yake watoe taarifa ili kuokoa maisha ya wengine.

Kwa upande wake, Ofisa wa TMDA, Idara ya Udhibiti wa Majaribio na Ufuatiliaji wa Usalama wa Dawa, Emanuel Masunga amesema miongoni mwa faida za kutoa taarifa ya maudhi au madhara ya dawa ni pamoja na kuangalia ubora kwani nyingine zinakuwa bandia au zimeingizwa nchini kwa njia za panya.

Amewataka wagonjwa watumie dawa kama walivyoelekezwa na daktari ili kuepuka madhara yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi.

Chanzo: Mwananchi