Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wahimizwa chanjo ya kipindupindu

3834d207b075796762200ca4d8918fc0.jpeg Wananchi wahimizwa chanjo ya kipindupindu

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANANCHI wa Kijiji cha Kiuyu Minungwini, Mkoa wa Kaskazini Pemba wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu bure, ambao mara kwa mara umekuwa ukisababisha vifo katika maeneo hayo na wilaya nzima ya Micheweni, Pemba.

Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Wete, Mgeni Khatib Yahya wakati akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo na shehia zake kuhusu chanjo ya kipindupindu.

Alisema mikakati ya serikali ya Zanzibar ni ifikapo mwaka 2030 kuona ugonjwa wa kipindupindu unakuwa historia na sio tishio tena kwa afya za wananchi.

Aliitaja wilaya ya Micheweni pamoja na kisiwa kidogo cha Kojani kuwa miongoni mwa maeneo ambayo mara kwa mara milipuko wa ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ukitokea na kusababisha vifo.

Ofisa wa Mradi wa Kinga na Afya Pemba, Iddi Mohamed Juma alisema wamejipanga kufanikisha chanjo ya kipindupindu awamu ya pili ambayo itamwezesha mtu kuwa na kinga ya ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka 10.

Alisema Wizara ya Afya inatoa chanjo hiyo kwa wananchi hasa katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa chanzo cha ugonjwa huo.

Alisema ugonjwa wa kipindupindu ni tishio zaidi kwa watoto, ambapo husababisha mtu kuharisha kwa wingi kwa wakati mmoja na mwili kupoteza maji mengi.

''Wananchi wa Wilaya ya Micheweni ikiwamo kisiwa kidogo cha Kojani mnatakiwa kujitokeza kwa wingi kupata chanjo awamu ya pili ya kujikinga na kipindupindu ambayo inatolewa bure,'' alisema.

Serikali ya Zanzibar inatoa chanjo ya kujikinga na kipindupindu kwa baadhi ya shehia za Unguja na Pemba, huku zaidi zikilengwa ambazo zimekuwa zikikumbwa na mlipuko wa maradhi hayo mara kwa mara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz