Wananchi wa Kijiji cha Kisawasawa Kata ya Kisawasawa Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro wamegoma kulipa bili ya maji ya elfu tano kwa mwezi wakidai ni kubwa.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo Dustan Kyobya wamesema hapo awali walikuwa wakilipa shilingi elfu mbili kwa mwezi Kwa wateja wasiotumia dira za maji lakini baadae wakapandishiwa bili hadi kufikia elfu tano.
Wananchi hao wamesema kuwa wakati mradi huo unajengwa walichangia shilingi milioni tano pia huwa wanatoa fedha za matengenezo pale panapo kuwa na hitilafu kwenye mifumo ya bomba zao.
Kufuatia hilo Mkuu wa wilaya hiyo Dastan Kyobya akamtaka meneja RUWASA wa Wilaya hiyo kujibu changamoto ya wananchi hao kupandishiwa bei ya bili ya maji kutoka elfu mbili hadi elfu tano ambapo meneja huyo alisema bei ilipanda ili kukidhi uendeshaji wa mradi huo.
Baada ya hayo yote Kyobya akatoa siku 60 kwa Meneja wa RUWASA pamoja na bodi ya maji ya kijiji hicho kufanya vikao na wananchi ili waweze kuangalia uwezekano wa kubadili bei hiyo.