Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wafurika banda la Nida Rorya, DC aingilia kati

Nida Nidaaaaa Wafurikaaaa.jpeg Wananchi wafurika banda la Nida Rorya, DC aingilia kati

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rorya. Mabanda ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Uhamiaji kwenye wiki ya huduma kwa wananchi wilayani Rorya yamezidiwa na wingi wa watu wanaohitaji huduma hio, hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya hiyo Juma Chikoka kuagiza maofisa zaidi wa taasisi hizo kufika kuongeza nguvu.

Mbali na maofisa hao mkuu huyo wa wilaya ameagiza kuongezwa kwa vitendea kazi ndani ya muda mfupi ili wananchi waliojitokeza kupata huduma wanazostahili ambapo zaidi ya watu 500 wameonekana kuwepo katika mabanda hayo mawili.

Hali hiyo imejiri leo Novemba 7, 2023 ikiwa ni siku ya pili kwa kambi ya huduma kwa wananchi ambapo wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri ya wilaya hiyo wamepiga kambi katika eneo la Shirati kwaajili ya kuwahudumia wananchi kwa muda wa siku tano.

Wakizungumza katika eneo hilo, baadhi ya wananchi wamedai muitikio huo unatokana na uhitaji wa huduma hasa za vitambulisho vya taifa.

"Ofisi ya uhamiaji ipo Shirati wakati ofisi ya Nida ipo Ingri sasa mzunguko unakuwa ni mkubwa unajikuta unatumia muda mwingi na gharama kubwa hivyo wengi wanashindwa kumudu gharama,"amesema William Alex mkazi wa kijiji cha Tai.

Modesta Ochieng' mkazi wa kijiji cha Omoche amesema upo uwezekano wa wananchi wengi kukosa huduma hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza ikilinganishwa na idadi ya watoa huduma waliopo.

"Ukiwafuata ofisini hawa watu mizunguko inakuwa mingi sana kwahiyo wengi waliposikia kuwa taasisi zote zitakuwa hapa wakaona ni nafasi kwao kupata huduma kwa ukaribu na nafuu,"amesema Jumanne Obuya

Kufuatia hali hiyo mkuu wa wilaya amesema nia ya serikali wilayani humo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote wanazostahili na kwa gharama nafuu.

"Kwenye mabanda haya ya Nida na Uhamiaji hali ndio kama hivyo mnavyoona ina maana uhitaji ni mkubwa sana zipo sababu zinazopelekea kuwepo kwa hali hii moja ni umbali wa zilipo huduma," amesema na kuongeza

"Sababu nyingine ni hali za kiuchumi kwani wananchi wanalazimika kutembea umbali mrefu au kutumia gharama kubwa kufuata huduma wilayani sasa kupitia programu hii tutahakikisha kila mwananchi anapata huduma kwa karibu,"

Amesema uhitaji wa vitambulisho vya taifa kwa wilaya ya Rorya ni mkubwa kufuatia muitikio wa watu hivyo na kuagiza ofisi ya Nida kupanga programu tofauti na hiyo iliyoandaliwa na ofisi yake ili kuwafikia wananchi na kuongeza kuwa vitambulisho vya taifa vina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya kawaida ya mwananchi.

Amesema kutokana na muitikio ulivyo katika eneo hilo ipo haja ya kuongeza wataalamu ili kila mmoja aliyejitokeza apate huduma anayohitaji kupitia programu hiyo ambayo imeingia awamu ya pili wilayani humo.

Katika awamu ya pili programu ya huduma kwa wananchi inatolewa kwa wakazi wa Tarafa ya Nyancha yenye kata 12 huku awamu ya kwanza iliyofanyika Mwezi Oktoba katika tarafa ya Suba zaidi ya watu 5,000 walijitokeza kupatiwa huduma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live