Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wafunga ofisi, wataka taarifa za mapato

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Wakazi wa mtaa wa Manga kata ya Mgusu halmashauri ya mji wa Geita wamefunga ofisi ya mtaa wakishinikiza mwenyekiti wa mtaa huo kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi.

Pia, wananchi hao wanapinga hatua ya ofisi ya Wakala wa Misitu (TFS) Geita kuwaondoa katika maeneo ya hifadhi wanakofanya shughuli zao za kilimo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo, Filipo Edward na Sabina Maziku walisema mwaka 2018 hawajasomewa taarifa ya mapato na matumizi na mwenyekiti amekuwa akifanya shughuli zake bila kuwashirikisha wananchi.

“Sisi tunaona majengo yanajengwa hatujui kwa kiasi gani lakini pia ametuletea watu sijui ndio TFS wameweka mahema wanatuzuia tusilime, hivi sisi tutakwenda kula wapi wakati haya ndio maisha yetu,” amesema Sabina.

Wananchi hao wamesema wameandika barua tangu mwaka jana ya kuomba kupewa maeneo hayo kwa ajili ya kilimo lakini hadi sasa hawajajibiwa na msimu wa kilimo umeanza.

Akizungumza katika mkutano ulioitishwa na ofisi ya mkuu wa wilaya kutafuta suluhu, mwenyekiti wa mtaa huo, Elias Lukanya  amesema mgogoro huo ni wa wananchi wachache wahamiaji ambao wamevamia maeneo ya hifadhi.

Meneja misitu wilaya ya Geita, Fredy Ndandika amesema wao kama TFS wamepewa mamlaka ya kusimamia misitu yote ya Serikali ikiwemo msitu wa Geita hivyo hawawezi kwenda kinyume na sheria.

Katibu tawala wilaya ya Geita, Janeth Mobe amewataka wananchi kutambua ofisi ni mali ya Serikali na si ya mwenyekiti hivyo waache kuchukua sheria mkononi na badala yake wafuate taratibu.

Chanzo: mwananchi.co.tz