Wananchi wa Kijiji Muwanda katika Bonde la Serenge, Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja wamelalamika kuwapo kikundi cha watu wasiojulikana walichodai kinawacharaza viboko bila sababu na kisha kutokomea kusikojulikana.
Wametoa madai hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohammed Mahmoud alipofika kusikiliza kero zao.
Vuai Said, mkazi wa kijiji hicho alisema kumeibuka watu ambao hawajulikani wanatoka wapi, lakini wamekuwa wakiwacharaza wananchi viboko na kusababisha taharuki kwenye jamii.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuna watu huwa wanatuchapa viboko bila sababu za msingi kisha wanatokomea, wakishafanya hivyo wanakimbia kusikojulikana,” alisema mkazi mwingine, Iddi Sultan.
Mkuu wa mkoa huo, Ayoub aliagiza Jeshi la Polisi la Mkoa huo kulifuatilia kwa umakini tatizo la kupigwa kwa wananchi wa kijiji hicho, jambo ambalo alisema linawakosesha amani ya kuishi.