Familia ya Salim Kivumbi, wilayani Handeni, Mkoan Tanga, imebidi kuingia mtaani kukusanya fedha, kwaajili ya kukomboa mwili wa mtoto Salehe Zuberi (5) ambaye kabla ya kufariki, alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akizungumzia suala hilo leo Novemba 16,2023 wilayani Handeni, mkoani Tanga, babu wa mtoto huyo Salim Kivumbi amesema wanadaiwa Sh2.4 milioni ambazo ni gharama za matibabu ya mtoto huyo.
Kivumbi amewaomba viongozi wa serikali na wananchi wasamalia wema kuisaidia familia hiyo kuweza kufanikiwa kupata mwili wa mjukuu wake kwaajili ya maziko kwa kuwa fedha wanayodaiwa, ni ngumu kwa familia hiyo kuwa nayo.
“Familia haina uwezo wa kuipata fedha hiyo, tunawaomba viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na wengineo waangalie ni jinsi gani wataweza kuisaidia familia hii kumpata mjukuu wangu na kumzika kwa heshima zote,” amesema.
Ameongeza kuwa umri wa mjukuu wake huyo bado ni mdogo sana, hivyo ombi lake ni kupewa huo mwili ili azike kwani hata ukizuiwa pesa inayohitajika familia yake hawataweza kuipata.
"Kwa Kiongozi anayehusika pale Muhimbili ombi langu namtaka yule mtoto mwenyewe, ni mdogo sana, sasa naona ajabu bili inazidi zaidi na yeye ni mdogo ana miaka mtano, sasa naomba serikali inisaidie iruhusu maiti ya huyu mjukuu nije nizike," amesema Kivumbi.
Akielezea kuhusu hali ya ugonjwa wa mtoto huyo hadi kukutwa na mauti, mama mkubwa wa marehemu Mariam Kivumbi amesema alipatiwa matibabu hospitali ya Handeni na baadae kuhamishiwa Muhimbili hadi kifo.
Amesema wakati wanaendelea na matibabu alishawaambia baadhi ya wahudumu kuwa maisha yao ni duni,na watahitaji kusaidiwa ila hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka mtoto anafariki.
Dada wa marehemu Shufaa Kivumbi amesema kuanzia Jumatano na Alhamisi tangu kutokea tukio hilo, wamezunguka mtaani na kufanikiwa kichangisha Sh150, 000 ila wameshaituma kwa wenzao waliopo Muhimbili.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Aminiel Aligaesha amesema hana taarifa kuhusiana na kuzuiwa kwa mwili huo, hivyo kuomba mawasiliano ya familia husika ili afuatilie.
Amesema kuwa atawasikiliza wazazi hao kujua walipatiwa vipi matibabu na madeni yake yakoje, ili kuangalia ataweza kuwasaidia vipi kwenye suala hilo.