Chama Cha Mapinduzi CCM kimemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Tanga kulipa fidia ya Shilingi Bilioni 1.7 kwa wananchi waliokua na viwanja eneo la stendi ya Kenge ambao bado hawajalipwa fidia zao.
Maagizo hayo ya CCM yametolewa na Katibu NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa Paul Makonda mara baada ya kuwasikiliza wananchi waliofika kutoa kero zao kwenye muendelezo wa ziara zake ambapo amesema baadhi ya watendaji wa umma wanaigombanisha serikali na wananchi kwakutowasikiliza wala kuwatatulia changamoto zao hasa sekta ya ardhi.
Katika ziara hiyo ya Makonda kumeibuka kero mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maji safi na salama ,miundombinu mibovu ya barabara, watu kudhulumiwa haki zao, huduma mbovu za hospitali na tatizo la kukatika kwa umeme hali ambayo ilimlazimu Mwenezi kuwasimamisha baadhi ya watendaji kujibu hoja za wananchi huku yeye akitoa ufafanuzi wa hatua zilizochukuliwa kupunguza tatizo la upungufu wa Nishati hiyo.
"Sio Tanzania pekee ndio kuna tatizo la upungufu wa umeme kwani kuna baadhi ya nchi pia tatizo hilo lipo kutokana na sababu mbalimbali ndio maana nchi ilipogundua hali hiyo iliamua kuweka chanzo cha umeme kikubwa na kujenga Bwawa la Umeme la Nyerere ambalo mwezi huu wa 1 kinu cha kwanza kinaanza kufungwa kwaajili ya majaribio na kila mwezi kulingana na matengenezo yanavyofanywa kitakua kinaingia na kuwekwa kinu kimoja hadi vifike vyote 8", alisema Makonda.
Kero alizosikiliza Mwenezi ambazo zimejirudia kila Wilaya aliyoenda ndani ya Mkoa wa Tanga ni dhuluma ya ardhi, kukatika nishati ya umeme, ukosefu wa maji safi na salama, ubovu wa barabara na vyote vinasababishwa na baadhi ya viongozi kutowasikiliza wananchi wao hali ambayo inaongeza mgongano kati ya serikali na wananchi.