Wakazi wa Misima na Mabanda katika Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, wameanza kuonja ‘neema’ ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), baada ya kuchimbiwa visima virefu viwili kwa ajili ya kuwasaidia kukabiliana na adha ya maji inayowakabili.
Hadi kukamilika kwa mradi huo, zaidi ya Watanzania 26,563, wanaopitiwa karibu na mradi huo, watanufaika na huduma ya majisafi na salama.
Meneja wa mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa ya JV SPEK, Arnold Siliro, alisema kazi ya ujenzi wa kambi ya Mabanda, hadi sasa umegharimu Sh. bilioni 8.9.
Kwa mujibu wa Siliro, mradi huo ulioanza Agosti 12, mwaka huu, umefikia asilimia 46 na unatarajiwa kukamilika Disemba 24.
“Tulifanya taratibu zote za matakwa ya kisheria na kupata vibali mapema ili tusipate matatizo baadae na tufanye kazi kwa muda. Mpaka sasa JV SPEK tuko kwenye asilimia 46.8 ya utekelezaji wetu,”alisema
Aidha, meneja huyo alisema walipofika eneo hilo, walikuta hapakuwa na maji ya kutosha, hivyo waliamua kuchimba visima viwili vinavyowatosheleza wananchi wa kata mbili na mengine kuwasaidia wananchi wa kata jirani.
Pia, alisema katika utekelezaji wao wamefanikiwa kufuata matakwa ya mkataba walioingia na serikali, kwa kuanza kulipa fidia wananchi wote ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi huo.
“Tutakapokuwa tumemaliza utekelezaji wa mradi wetu na kuondoka, basi visima hivi tutawaachia wananchi wa Mabanda na watu wa Handeni, kwa sababu haya maji yaliyopo hapa, yanaweza kutosheleza watu wengi,” alisema.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Mwajuma Ukwaju, alisema mradi huo umekuwa chachu kwa Wilaya hiyo, kwa kuwa mji umekua kibiashara na kuchangia kuongeza mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba, alisema mradi huo sio tu, utafungua fursa za Wilaya ya Handeni, bali pia Mkoa kwa ujumla wake.
Hata hivyo, Mgumba, alidokeza kuwa mradi huo pia utazinufaisha Wilaya za Handeni, Kilindi, Muheza, Korogwe, Tanga, na Mkinga.
Aliishukuru kampuni hiyo, kwa kuelezwa mkataba wao wa kutumia watu na vitu ndani ya wilaya husika kwa kutoa ajira kwa vijana huku akiwasisitiza kuendelea kuzingatia mkataba huo kwa kufanya kazi nzuri itakayo wawezeaha kuonekana na kupewa kazi nyingine inapotokea uhitaji.