Dar es Salaam. Waziri wa Tamisemi nchini Tanzania, Suleiman Jafo amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Jafo ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 4, 2019 akiwataka wananchi hao kujiandikisha ili kupata haki yao ya msingi kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.
Akizungumza mjini Vwawa mkoani humo katika siku ya kwanza ya ziara ya siku tatu ya Rais wa Tanzania, John Magufuli, waziri huyo amesema wananchi wataanza kujiandikisha kwenye daftari hilo kuanzia Oktoba 8, 2019.
“Nihamasishe wananchi wa Songwe mjitokeze kujiandikisha kwa wingi katika orodha ya wapiga kura ili muweze kupata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo,” amesema Jafo.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Mkoa huo, Jafo amesema Serikali imefanikiwa kujenga hospitali tatu ikiwamo ya mkoa wa Songwe na kuboresha vituo vya afya nane.
Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Songwe umeanza na tayari wameshaingiza fedha Sh2.2 bilioni.
Habari zinazohusiana na hii
- Magufuli aagiza Sh100 milioni kuongezwa mradi wa maji Vwawa
- Magufuli agiza wananchi kutochangishwa Sh25,000 mkoani Songwe
- Magufuli afungua jengo la mahakama kiaina
- Rais Magufuli amaliza mgogoro wa ardhi eneo la ekari 2,115