Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Simanjiro kucharazwa viboko 70

12356 Pic+viboko TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simanjiro. Wananchi wa kijiji cha Terrat wilayani  Simanjiro mkoani Manyara watakaokata miti, kutupa taka na kulishia mifugo kwenye chanzo cha maji cha Mto Terrat watacharazwa viboko 70.

Adhabu hiyo imetokana na wazee wa kimila wa jamii ya wamasai kupitisha sheria baada ya kutokea uharibifu wa mazingira kwenye mto huo na kusababisha maji kukauka.

Mmoja wa wazee wa kimila wa eneo hilo, Leshule Lesindiya akizungumza jana Alhamisi Agosti 16, 2018 amesema wamepitisha sheria hiyo kwa mtu atakayekiuka maagizo hayo kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kutunza mazingira ya eneo hilo.

Amesema wanaishukuru Serikali kwa kuridhia utekelezaji wa sheria hiyo ndogo ambayo kwa namna moja au nyingine itawasaidia wananchi wa eneo hilo kuepuka uharibifu wa mazingira uliokuwa ukifanyika.

"Awali ilionekana kama ni ubabe pindi mtu akipatiwa haki yake ya msingi ya kuchapwa viboko 70 kwa kuharibu mazingira lakini sasa wananchi wameeleweshwa na mtu akikosea anakubaliana na adhabu hiyo kwani si kwa ajili ya kuonewa ni kosa lake mwenyewe,"amesema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Terrat, Godson Nduya amesema Mto Terrat ni mto wa asili kwenye wilaya ya Simanjiro unaohudumia zaidi ya wananchi wa vijiji saba.

Nduya amesema vyanzo vya maji vilivyokuwa vinasaidia mto huo kuwa na maji nyakati za kiangazi na masika ni miamba ya asili yenye chemchem inayotiririsha maji kila wakati.

Amebainisha kuwa uwepo wa maji kwa kipindi chote cha miaka ya nyuma ni kutokana na kuwa na mimea asili ambayo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kutunza na kuhifadhi mto ila hivi sasa sehemu kubwa ya miti hiyo imekatwa.

Mkazi wa kijiji hicho, Joseph Lengenyu amesema sheria hiyo kwa namna moja au nyingine itachangia wananchi kuheshimu mazingira na kuyatunza kwani bila kuchukuliwa hatua hakuna kitu kitafanyika.

Chanzo: mwananchi.co.tz