Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Shinyanga walia mikopo umiza, vicoba kuvunja ndoa

Vicoba P Ic Wananchi Shinyanga walia mikopo umiza, vicoba kuvunja ndoa

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wananchi wa Mtaa wa Dome uliopo manispaa ya Shinyanga wamemuomba Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi kusimamia suala la mikopo umiza kwa wanawake kwani limekuwa likisababisha ndoa nyingi kuvunjika na kusababisha watoto kuishi katika mazingira magumu.

Wameeleza hayo leo Desemba 30, 2022 kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na mwenyekiti wa mtaa huo ambapo mgeni rasmi alikuwa Magomi Wananchi hao wamesema hali ni mbaya kwa baadhi ya familia ambazo zinadaiwa marejesho kwa sababu wengine wamekimbia familia zao kwa kukosa marejesho hayo.

Mkazi wa Mtaa wa Dome, Adelta Maleo amesema mikopo midogo midogo imekuwa ikivunja familia na wengine kutelekeza familia.

Amesema wanawake wamekuwa wakikimbilia mkopo kila kona na kushindwa kurejesha marejesho, hali ambayo imekuwa ikiwasababisha kukimbia madeni huku ndoa zikivunjika kisha kutelekeza watoto.

“Tunakuomba kamanda wetu utusaidie kwa hili maana mama anakwenda kukopa mkopo wa leo leo lakini hajui fedha hizo anazipeleka wapi. Anakopa hata mume wake hajui, anapokosa marejesho wanaodai wanakuja moja kwa moja hadi kwa mwanaume kudai.

“Anaposikia hivyo, mwanaume ndani inakuwa ugomvi mkubwa na kuvunjika ndoa tu, naomba ulisimamie suala hilo,” amesema Maleo.

Charles Mpinga ambaye ni mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mtaa wa Dome, amesema kila sehemu kumekuwa na ofisi za mikopo, wanataka zichunguzwe kama zitakuwa na kibali maana inawezekana hata hawana vibali lakini wanasumbua watu kwa kudai marejesho.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Solomon Najulwa amesema mpaka sasa ana taarifa ya wanawake tisa wamekimbia familia zao kutokana na kukosa marejesho, wengine wanakwenda kukopa kwa ajili ya kufaulisha mikopo.

“Mikopo hii imekuwa ikisababisha kina baba kukosa raha kwa sababu wakitaka tendo la ndoa, wanajibiwa ‘niache mimi ninarejesho’. Hivyo, tumeacha maandiko matakatifu ndiyo maana wamekuwa wakihangaika na marejesho, wakati mwingine wanafuatwa wanaume ama nafuatwa mimi kuombwa marejesho, jamani nihurumieni mtoto wa mwanamke mwenzenu,” amesema Najulwa.

Kwa upande wake, kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Magomi amesema atalifanyia kazi suala hilo na ataongozana na ofisa biashara wa mkoa ili kuzitambua ofisi hizo za ukopeshaji kama zitakuwa zinafanya kazi kwa utaratibu unaotakiwa.

Chanzo: Mwananchi