Wakazi zaidi ya 2,000 wa Kijiji cha Remung'orori Wilaya Serengeti mkoani Mara wamefunga ofisi, na kutangaza azimio la kutoshiriki shughuli za maendeleo kama njia ya kushinikiza utatuzi wa mgogoro wa mpaka kati ya kijiji hicho na Kijiji cha Mekomariro Wilaya ya Bunda.
Mgogoro wa mpaka kati ya vijiji hivyo viwili umedumu tangu mwaka 2014 baada ya Serikali kutangaza na kuweka alama mpya wa mipaka huku baadhi ya maeneo yakiwemo mashamba ya kaya 18 kutoka Kijiji cha Remung’orori kuhamishiwa Kijiji cha Mekomariro.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kufunga ofisi ya Serikali ya kijiji, wananchi hao walifanya maandamano ya amani kwa kuzunguka maeneo tofauti ya kijiji kama ishara ya kufikisha ujumbe wa kuchukizwa na kitendo cha mgogoro huo kutotatuliwa licha ya taarifa kufikishwa kwenye mamlaka tofauti za Serikali kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi mkoa.
Maandamano hayo ya amani yalifanyika kijijini hapo Julai 25, 2023 na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara ambao pia ulihudhuriwa na kuhutubiwa na viongozi wa Serikali ya kijiji na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Remung’orori ambao walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao.
‘’Viongozi wa kijiji na wenzao wa CCM wamekosa sifa za kusalia kwenye nafasi zao; wameshindwa kutafutia ufumbuzi mgogoro wa mpaka kati ya kijiji chetu na kijiji cha Wilaya jirani ya Bunda. Tumeazimia kufunga ofisi ya Serikali ya kijiji na hatutashiriki shughuli yoyote ya maendeleo hadi suala hili litatuliwe,’’ amesema Debora Zakaria, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Remung’orori
Kijiji cha Remung’orori chenye wakazi zaidi ya 7, 000 kilianzishwa mwaka 1974 na kusajiliwa kwa namba MR/KJ/86.
Wambura Magori, mkazi mwingine wa kijiji hicho, anasema tangu wakati huo, wameishi kwa amani na utulivu na wenzao wa Kijiji cha Mekomariro hadi Serikali ilipotangaza na kuweka alama mpya ya mpaka uliosababisha mashamba ya kaya 18 kutoka Kijiji cha Remung’orori kuhamia kijiji jirani cha Mekomariro.
‘’Hivi sasa wenzetu wa Kijiji cha Mekomariro hawaturuhusu kulima mashamba yetu ya asili tuliyorithi kutoka kwa baba na babu zetu. Hili ni tatizo kubwa na juhudi zote kutafutia ufumbuzi suala hili katika ofisi zote za Serikali zimegonga mwamba,’’ amesema Wambura
Msimamo mkali wa wananchi wakati wa maandamani na baadaye kwenye mkutano wa hadhara umewalazimisha viongozi wote wa Serikali ya kijiji kutangaza kuachia ngazi kutoa fursa kwa viongozi wapya kuchaguliwa.
Uamuzi huo wa kuachia ngazi umetangazwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Hezron Msamba na kuungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Remung'orori, Masisi Maro ambaye pia ametangaza kujiuzulu nafasi yake baada ya wananchi kuonyesha kukosa imani na viongozi wa chama hicho tawala.
Ofisa Mtendaji Kijiji cha Remung’orori, David Makonda amesema japo shughuli na huduma za kiserikali zinaendelea kutolewa, kitendo cha wananchi kufunga ofisi kina madhara kiuongozi kwa sababu watendaji wanalazimika kufanya shughuli zao nje ya ofisi.
‘’Wananchi wamekoswa uvumilivu. Mkuu wa Wilaya ya Serengeti tayari amefika hapa karibia mara nne katika jitihada za kulitafutia ufumbuzi suala hili. Nawasihi wananchi waendelee kuwa wavumilivu na watulivu wakati Serikali inashughulikia tatizo hili,’’ amesema Makonda
Katika hatua nyingine, mtendaji huyo wa kijiji amewaonya wananchi dhidi ya nia ya kuwazuia watoto wao kwenda shule kama njia ya kuishinikiza Serikali kutatua tatizo hilo akisema kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kunaweza kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria kwa kuwanyima watoto haki ya elimu.
‘’Nawataka wazazi na walezi wasiwazuie watoto wao kwenda shule kwa sababu kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kutawafikisha mahakamani,’’ ameonya mtendaji huyo wa kijiji
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vincent Mashinji amethibitisha kupokea taarifa za wananchi kufunga ofisi ya kijiji na viongozi wote kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao akisema uongozi wa wilaya unasubiri taarifa rasmi kabla ya kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuitisha chaguzi ndogo kujaza nafasi zilizoachwa wazi.
"Hoja zote zilizotolewa na wananchi kuhusu mgogoro wa mpaka kupitia vikao rasmi tayari zimetolewa ufafanuzi. Walituambia kuna wananchi ambao makazi yao yako Wilaya ya Serengeti huku mashamba yao yako Kijiji cha Mekomariro Wilaya ya Bunda; hilo nalo tunalifanyia kazi,’’ amesema Dk Mashinji
Amesema hata hoja yao ya kuomba kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Mara tayari imewasilishwa kwa kiongozi huyo ambaye pia amekubali kupanga muda wa kwenda kijijini hapo kuzungumza nao, hivyo kuwataka wananchi kuwa wavuilivu na watulivu.
‘’Ninachowaonya ni kutofanya jaribio lolote la uharibifu wa mali au kuvunja amani kwa sababu kufanya hivyo ni kukiuka sheria na kutailazimisha Serikali kuchukua hatua stahiki,’’ amesema na kuonya DC Mashinji
Kuhusu suala la mipaka, Mkuu huyo wa wilaya amesema hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kurekebisha hilo isipokuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa (Tamisemi) baada ya kupokea maombi, maoni na mapendekezo ya vikao na mamlaka tofauti kuanzia ngazi ya vijiji, kata, wilaya na mkoa.