Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Ruangwa wafurahia zahanati kupandishwa hadhi

67846 Pic+wananchi

Mon, 22 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Wakazi wa kata ya Mbekenyera wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi nchini Tanzania sasa wataondokana na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya katika hospitali ya wilaya lakini pia kupunguza gharama za usafiri na malazi kwa ndugu wa wagonjwa.

Unafuu huo unakuja baada ya zahanati ya kijiji cha Mbekenyera kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya sambamba na kuongezwa kwa majengo mbalimbali kama jengo la huduma za mama na mtoto, maabara, chumba cha upasuaji, sehemu ya kuhifadhi maiti na sehemu maalumu ya kuchoma taka.

Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2012 kata hiyo ilikuwa na wakazi wapatao 11,257.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 22, 2019 mkazi wa kijiji cha Mbekenyera, Sophia Andrew amesema kabla wajawazito walilazimika kwenda kupata huduma katika hospitali ya wilaya Ruangwa na waliozidiwa njiani kutokana na barabara kutokuwa nzuri walipatwa matatizo zaidi.

“Kwa kweli tunaishukuru sana serikali kwa sababu zamani tulikuwa hatuna huduma  hasa kwa mama anapotaka kujifungua, ilikuwa lazima kwenda wilayani ambapo gharama za usafiri zilikuwa kubwa wakati wa kokodi usafiri hasa ikiwa usiku, wakati mwingine mama aliweza kujifungulia njiani,”amesema Andrew

Diwani wa  viti maalum, Zainabu Abdallah amesema zahanati hiyo hata kabla ya kupandishwa hadhi ilikuwa ikitegemewa na kata nne na sasa imekuwa nafuu baada ya kupandishwa hadhi na huduma kuanza kuboreshwa.

Pia Soma

“Tunashukuru sana kwa sababu zamani ilikuwa adhabu, hakuna mimba zilizokuwa rahisi kuzaliwa hapa (Mbekenyera) ilikuwa lazima Ruangwa lakini sasa hivi ukiona mama ameshindwa kujifungulia hapa ujue ni tatizo kubwa,” amesema Abdallah

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Ernest Ntagaye amesema licha ya kwamba bado hawajaanza huduma za upasuaji, tayari wana jengo la huduma za mama na watoto ambalo limeanza kutumika  kwani awali lilikuwepo jengo la kliniki za kawaida na chanjo ambalo liligawanywa na kupatikana chumba kwa ajili ya kujifungulia.

“Kulikuwa na chumba ambacho tumekitenga kwa ajili ya kujifungulia tofauti na majengo ya sasa ambayo kuna vyumba vya kujifungulia vya kisasa, lakini kuna vyumba baada ya kujifungua kawaida na upasuaji, pia kuna chumba kwa ajili ya watoto njiti lakini ambacho hakijaanza kufanya kazi sababu bado hatujapata vifaa,” amesema Dk Ntagaye

Aidha amesema katika jengo la mama na watoto bado hawajapata vifaa na kwamba wanatumia vifaa kama vitanda vya zamani kwa ajili ya kutoa huduma.

Chanzo: mwananchi.co.tz