Wananchi wa Kata ya Katangara Mrere, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii kuwapa kibali cha kuwaruhusu kuua nyani kwenye maeneo hayo baada ya kuwa kero kwenye makazi yao.
Nyani hao ambao hutembea makundi kwa makundi nyakati za asubuhi na jioni wanadaiwa kuwa ni tishio katika jamii zinazoishi pembezoni mwa mto Mlembea na maeneo ya tambarare wilayani humo.
Hivi karibuni baadhi ya wanaume wilayani humo, walilivalia njuga suala la nyani hao mbele ya Mbunge wao, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara kata ya Kirongo Samanga wakimweleza wamechoka na nyani hao.
Wakizungumza leo Februari Mosi katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika kijiji cha Katangara, wilayani humo, wananchi hao wameiomba Serikali kuwaruhusu kutumia nguvu zao wenyewe ili kuwaondoa nyani hao kwenye makazi yao kuwa wamekuwa ni waharibifu.
Anicet Silayo, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, amesema wanaogopa kuwaua nyani hao kwa kuwa hawana kibali, hivyo wakaiomba Serikali kupa nafasi ya kupambana nao wenyewe kuwa nyani hao hawana faida kwao.
"Nyani hawa wamekuwa ni kero sana, tunatamani Serikali itupe kibali tupambane nao wenyewe, hawatatushinda, kwa miaka mingi tumekuwa tukipambana na hawa nyani kuwafukuza kwenye maeneo yetu lakini hawaondoki, imefika mahali hata kulima hatulimi tena kwa sababu ya hawa nyani wanakula mazao yetu," amesema.
Kwa upande wake Amadea Stambuli, mkazi wa Kata hiyo, amesema nyani hao wamekuwa ni tishio kubwa kwenye makazi ya wananchi kutokana na wingi wao kwenye makazi yao na kwamba imefika mahali nyani hao huingia ndani na kula vyakula vilivyopikwa.
"Ukipika chakula, ukisahau kufunga mlango kama haupo nyani wanaondoka nacho, kwa kweli wamekuwa ni kero mno, wamekuwa wakila mifugo yetu, wanaharibu mazao mashambani imefika mahali tumechoka.
“Serikali itupe ruhusa wananchi tuungane pamoja ili tuwaangamize hawa nyani wenyewe," amesema.
Maombi hayo ya wananchi yaliungwa mkono na Diwani wa kata hiyo, Venance Mallel ambapo aliyesema wapo tayari kupambana na nyani hao, kwa kuwa wamekuwa ni wasumbufu na ni waharibifu