Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Rombo walia kubomolewa nyumba kupisha barabara

Bomoa1 Wananchi Rombo walia kubomolewa nyumba kupisha barabara

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mbomai kilichopo kata ya Tarakea Motamburu, wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wanalazimika kulala nje baada ya nyumba zao kubomolewa kupisha ujenzi wa barabara ya Msikitini kwa Zuberi inayojengwa kilomita moja kwa kiwango cha changarawe.

Wananchi hao wamemwomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati mchakato huo, kwani hawakushirikishwa chochote kuhusu suala la upanuzi wa barabara hiyo wala kupewa notisi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, wananchi hao ambao nyumba zao zaidi ya sita zimebomolewa, wamesema kilichofanyika ni uonevu kwa kuwa hawakupewa taarifa yoyote ya maandishi wala maeneo yao kuwekwa alama ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

Felix Ndetembea, mkazi wa kijiji hicho ambaye nyumba yake imebomolewa, amesema kilichofanyika ni uonevu kwa kuwa hawakupewa taarifa kuhusu nyumba zao kuvunjwa.

“Hakuna mwenyekiti wala balozi aliyetutaarifu kuhusu hili jambo linaloendelea hapa, nilishangaa tu kuona haya magari yanayochimba barabara yanavunja nyumba yangu, nimebaki sina mahali pa kulala nimehangaika usiku na mchana sijapata msaada wowote.

“Nilimfuata mwenyekiti wangu wa mtaa hakusaidia chochote, sina msaada wowote hapa nilipo na maisha yangu ni ya kubangaiza, namwomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie sisi wananchi wa hali ya chini, aone jinsi tunavyonyanyasika huku mtaani,” amesema mwananchi huyo.

Mkazi mwingine wa Mbomai ambaye nyumba yake yenye vyumba sita imebomolewa, Arobogast Silayo amesema kilichofanyika ni kuwaumiza wananchi wa hali ya chini kwa kuwasababishia hasara kwa jambo ambalo hawakushirikishwa.

“Tumevunjiwa maeneo yetu bila taarifa yoyote hata ya maandishi. Nyumba yangu ya vyumba sita ilikuwa kwenye hatua ya upauaji ambapo nimeshatumia  zaidi ya Sh16 milioni, hii fedha nitaipata wapi tena, hii ni hasara.”

“Wananchi tunateseka sana, sisi sio kwamba hatutaki maendeleo, tunapenda sana, shida iliyopo kwa viongozi wetu ni kwamba hawatushirikishi chochote, huu ni uonevu hasa kwa sisi wananchi wa hali ya chini, tunaomba Serikali iangalie hili jambo,” amesema mwananchi huyo.

Monica Massawe, mkazi wa kijiji hicho, ameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kutokana na wengi wao kuwa na hali za chini na kilichofanyika kwao ni anguko kubwa kwa kuwa wamejenga nyumba zao kwa taabu.

“Juzi asubuhi nilikuwa nimetoka barabarani nikakutana na mwenyekiti, akaniambia watavunja nyumba yangu, nikamuuliza mbona hamjatoa taarifa akasema taarifa imeshatolewa na Serikali, kweli walifika kwenye nyumba yangu na kuanza kuvunja, hapa nilipo sina sehemu ya kulala na nyumba yangu nilijikusanya kwa miaka 15 kuijenga, nilipo sina biashara, mume na nina watoto watano sijui nitaishije,” amesema mama huyo.

Ameongeza: “Namwomba Mama Samia Suluhu Hassan atusaidie na atuangalie kwa jicho la huruma, aone namna ambavyo wananchi wake huku vijijini tunavyoteseka.”

Kwa upande wake, Justine Shirima amesema, “Sisi wananchi hatujakataa maendeleo yafanyike katika maeneo yetu, lakini tulipaswa kupewa taarifa rasmi kwamba kuna jambo litafanyika, tunashangaa tuu ghafla watu tunavunjiwa nyumba pamoja na miti kwenye maeneo yetu bila taarifa, kilichofanyika ni uharibifu mkubwa kwetu na ni hasara.”

Alipoulizwa kuhusu shughuli hiyo ya ujenzi wa barabara, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Mkoa wa Kilimanjaro,  Nicholus Francis amesema baada ya uongozi wa kijiji na kata kukubaliana kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, waliendelea na shughuli yao ya upanuzi kama kawaida.

“Hiyo barabara ni kweli tunajenga sisi Tarura, uongozi wa kata na kijiji husika walikubaliana wote, kwa hiyo sisi tunachofanya tumegusa yale maeneo ambayo wananchi wameingia kwenye hifadhi ya barabara zetu,” amesema Francis.

Alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo, mkuu wa wilaya hiyo, Raymond Mwangwala amesema atafika kijijini hapo pamoja na timu yake kuona kimetokea na kusema suala la kubomoa nyumba ya mtu bila taarifa sio sahihi.

“Nitatuma timu iende ikaangalie kuna shida gani, kwa sababu huwezi ukambomolea mtu nyumba, nitafika eneo husika nione nini kimetokea, maana kabla ya kufanya hilo jambo ni lazima wananchi wawe wameshirikishwa kwa maana ya kila kitu kiwe ni shirikishi, sio mtu aende akatumie nguvu,” amesema DC Mwangwala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live