Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Ngara walia kukosa namba, vitambulisho vya Taifa

IMG 4970.jpeg Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa hadhara

Sun, 23 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakazi wa Kata ya Ntobeye Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamefikisha Kilio cha kukosa namba na vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa mbunge wao, Ndaisaba Ruhoro wakimwomba awasaidie kumaliza tatizo hilo.

Wananchi hao wamewasilisha kilio chao wakati wa mkutano wa hadhara uliyofanyika Kijiji cha Kigina Julai 22, 2023 wakisema kukosa namba na vitambulisho vya NIDA siyo tu huwakwamisha kupata huduma katika ofisi za umma, bali pia kupata mitaji kutoka taasisi za fedha kupitia mikopo na miamala ya fedha kwa njia mtandao.

"Baadhi yetu wameshindwa hata kupata leseni za biashara kwa kukosa namba au kitambulisho cha Taifa wakati wa kuomba namba ya mlipakodi (TIN) kutoka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania). Serikali lazima itusaidie kuondokana na tatizo hili," amesema Annastazia John

Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Ntobeya, Sande Mkozi kati ya wakazi zaidi ya 25, 000 wa kata hiyo, ni watu wasiozidi 500 ndio wamefanikiwa kupata vitambulisho vya Taifa huku wengine zaidi ya 2, 000 wakiwa na namba.

Kata ya Ntobeya ni miongoni mwa kata za Wilaya ya Ngara zinazopakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi zenye changamoto ya uraia kwa wakazi wake kama ilivyo kwenye maeneo mengi ya mipakani nchini.

Kata hiyo iko umbali wa takribani kilometa 15 kutoka mjini Ngara iliko Makao Makuu ya Wilaya, hali inayowalazimisha wananchi kutumia gharama kubwa kufuatilia namba na vitambulisho vya Taifa katika ofisi za NIDA.

‘’Tunatumia gharama ya Sh20, 000 kukodisha pikipiki kwenda na kurudi ofisi za NIDA mjini Ngara kufuatilia namba au vitambulisho vya Taifa. Tunakusihi mbunge wetu utusaidie wananchi wenye sifa ambao tumekamilisha taratibu tupate vitambulisho au namba," amesema Heziron Bisekwa, mkazi wa kijiji cha Kigina Kata ya Ntobeye

Akizungumza na wananchi hao, mbunge Ruhoro ameahidi kutatua kero hiyo huku akiwaomba wote waliosajiliwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao pindi maofisa wa NIDA na Uhamiaji wanapofika kwenye maeneo yao.

"Kuna tatizo la wananchi kutojitokeza maofisa wa NIDA na Uhamiaji wanapofika kufanya uhakiki kwenye maeneo yao. Mwaka 2021 na 2022 niliwaleta maofisa wa NIDA na Uhamiaji hapa Kata ya Ntobeye lakini ni watu wachache tu ndio walijitokeza kuhakiki taarifa zao," amesema mbunge Ruhoro

Huku akiahidi kuwapeleka tena maofisa wa NIDA na Uhamiaji katika Kata ya Ntobeye mwakani, mbunge huyo amewasihi wananchi wanaodai haki ya kupata namba na vitambulisho vya Taifa nao kutimiza wajibu wao wa kujitokeza kuhakikiwa taarifa zao.

Mbunge huyo anaendelea na mikutano ya hadhara jimboni kwake kusikiliza, kukusanya na kutatua kero za wananchi.

Chanzo: Mwananchi