Wananchi wa Mkoa wa Mtwara wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwepo wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini mkoani humo.
Akizungumza leo katika mahojiano maalum na Afisa wa Idara ya Habari- MAELEZO, Bw. Maulid Mohamed mkazi wa Mitengo, Manispaa ya Mtwara Mjini, anasema kuwa uwepo wa hospitali hiyo umewasaidia kupata huduma za afya karibu na makazi yao kuliko ilivyokuwa awali
“Unajua huko nyuma mgonjwa akihitaji matibabu ya kibingwa ilitulazimu kwenda Dar es salaam. Sasa katika hospitali hii tunapata huduma nzuri na mimi nafurahia pia uwepo wa vifaa vya kisasa, tunaishukuru sana Serikali,” anaeleza Bw. Mohamed.
Kwa upande wake, Bi. Mariam Ngulangwa, mkazi wa Ligula, Mtwara Mjini, anasema kuwa awali walikuwa wanatibiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Ligula.
“Tunakuja huku sasa kwa kuwa hii ni hospitali mpya na ina huduma nyingi na nzuri sana. Namshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii ya Rufaa Kanda ya Kusini na sasa hakuna haja ya kwenda mbali, hapa hapa tunapata matibabu ya kibingwa,” amebainisha Bi. Mariam.
Daktari wa hospitali hiyo, Brian Buberwa, ameeleza kuwa uwepo wa hospitali hiyo unawasaidia kwa kiasi kikubwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi pamoja na nchi jirani za Msumbiji na Visiwa vya Comoro kwa kupata matibabu.
“Pia, hapo mwanzo tulikuwa na madaktari waliosoma kwa ngazi ya stashahada lakini kwa sasa kuna madaktari wa ngazi ya shahada ya kwanza na wengine ni madaktari wabobezi hivyo imesaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma zetu,” amefafanua Daktari. Buberwa.
Ameongeza; “Uwepo wa matibabu ya kibingwa bobezi yameweza kutusaidia kugundua magonjwa na kuyatibu mapema, na hivyo wagonjwa wetu hawahitaji tena kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.”
Halikadhalika, Daktari wa Tiba Vitendo, Hussein Hamka ameeleza kuwa yeye amepata ajira kupitia hospitali hiyo na hivyo inamsaidia kutunza familia yake sambamba na kusaidia wagonjwa.
“Binafsi, namshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kuwa hapa naweza kufanyia kazi ujuzi wangu, pia tunatumia vifaa vya kisasa kutoa huduma zetu,” ameeleza Daktari Hamka.